📌 Mitungi ya gesi 3,255 kusambazwa na kuuzwa kwa bei ya ruzuku
📌Mtungi mmoja kuuzwa kwa bei ya ruzuku ya shilingi 17,500
MANYARA-Wakala wa Nishati Vijijini (REA) tarehe 21 Januari, 2026 umeendelea na usambazaji na uuzaji wa mitungi ya gesi ya kilo sita kwa bei ya ruzuku wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara.
Uuzaji na usambazaji umefanyika katika kata ya Mirerani maeneo ya ofisi ya mamlaka ndogo ya mji wa Mirerani.
Akizungumza wakati wa uuzaji wa mitungi hiyo msimamizi wa mradi kutoka REA, ndugu Abdulrazack Mkomi amesema,usambazaji na uuzaji wa mitungi ya gesi ya kilo sita kwa bei ya ruzuku ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia uliozinduliwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mwezi Mei,2024.
Aidha, amesema mkakati huo wa nishati safi ya kupikia unaotekelezwa na Serikali ya Awamu Sita una lengo mahususi la kuboresha maisha ya wananchi kwa kuhakikisha ifikapo 2034 asilimia themanini (80) ya watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.
Vilevile, amesema nishati hiyo safi ya kupikia itasaidia katika uimarishaji na utunzaji wa afya za wananchi, kutunza mazingira na kuleta usawa wa kijinsia katika jamii.
Aidha, mradi huo utazambaza na kuuza Mitungi ya gesi 3,255 ambapo mtungi mmoja utauzwa kwa bei ya ruzuku ya TZS 17,500 na mwananchi atatakiwa kuja na kitambulisho cha Taifa (NIDA).
Halikadhalika, wananchi wa kata ya Mirerani wameipongeza na kuishukuru Serikali na REA kwa kuwezesha upatikanaji wa mitungi ya gesi pamoja na usimamizi mzuri wa mradi na kuahidi kutumia fursa ya upatikanaji wa mitungi ya gesi ya ruzuku kujiletea maendeleo na kuboresha ustawi wa maisha yao.


























