Tanzania na Hungary kuimarisha ushirikiano wa kimaendeleo


SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepongeza hatua ya Hungary kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi na Tanzania, hasa kupitia utekelezaji wa miradi ya maji na maendeleo ya kijamii.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, akiteta jambo na Kaimu Balozi wa Hungary Nchini, Mhe. David Tòth (Katikati), baada ya kukutana na kufanya mazungumzo kuhusu kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi na Tanzania, hasa kupitia utekelezaji wa miradi ya maji na maendeleo ya kijamii, katika Ofisi za Wizara ya Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma. Kushoto ni Mtaalamu wa Miradi ya Maji, Wizara ya Mambo ya Nje na Biashara ya Hungary, Bw. Szabolcs Nagy.

Pongezi hizo zimetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, alipokutana na kufanya mazungumzo na Kaimu Balozi wa Hungary Nchini, Mhe. David Tòth, katika Ofisi za Wizara ya Fedha, jijini Dodoma.

Dkt. Mwamba aliishukuru Serikali ya Hungary kwa mchango wake mkubwa katika kukuza uhusiano wake na Tanzania, hasa kwa hatua ya hivi karibuni ya kufungua Ofisi ya Kidiplomasia jijini Dar es Salaam ambayo ni ishara ya dhamira ya dhati ya nchi hiyo katika kuimarisha uhusiano na Tanzania.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (kulia), akimkabidhi zawadi Kaimu Balozi wa Hungary Nchini, Mhe. David Tòth, baada ya kukutana na kufanya mazungumzo kuhusu kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi na Tanzania, hasa kupitia utekelezaji wa miradi ya maji na maendeleo ya kijamii, katika Ofisi za Wizara ya Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma.

Aliongeza kuwa Serikali ya Tanzania inaithamini sana dhamira ya Hungary katika kufadhili miradi ya maendeleo ikiwemo Mradi wa Maji wa Biharamulo katika Mkoa wa Kagera, unaoendana kikamilifu na vipaumbele vya maendeleo ya Taifa vilivyoainishwa katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22–2025/26) pamoja na Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, akizungumza jambo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Kaimu Balozi wa Hungary Nchini, Mhe. David Tòth (hayupo pichani), katika Ofisi za Wizara ya Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma, ambapo aliishukuru Serikali ya Hungary kwa mchango wake mkubwa katika kukuza uhusiano wake na Tanzania, na pia kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi, hasa kupitia utekelezaji wa miradi ya maji na maendeleo ya kijamii.

“Utekelezaji wa mradi huu utaboresha huduma za maji safi kwa wananchi wa Biharamulo na maeneo jirani, na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii,” alisisitiza Dkt. Mwamba.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban na Kaimu Kamishna wa Idara ya Uchambuzi wa Sera, Dkt. Remidius Ruhinduka, wakifuatilia mazungumzo ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba na Kaimu Balozi wa Hungary Nchini, Mhe. David Tòth (hawapo pichani), walipokutana katika Ofisi za Wizara ya Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma, ambapo walijadiliana kuimarisha zaidi ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi na Tanzania, hasa kupitia utekelezaji wa miradi ya maji na maendeleo ya kijamii.

Vilevile, Dkt. Mwamba alihimiza upanuzi wa mfumo wa ushirikiano wa kifedha kati ya Tanzania na Hungary ili kuhusisha pia misaada ya ruzuku (grant) kwa miradi ya kijamii na kiuchumi.

“Tunaishukuru Hungary kwa mikopo nafuu, na mfumo wa ushirikiano wa sasa kati ya nchi zetu umejikita zaidi katika mikopo nafuu, huku ukiwa na nafasi ndogo ya ufadhili wa ruzuku tungependa kuona upanuzi wa mfumo huu ili kujumuisha pia misaada ya ruzuku katika sekta muhimu za kipaumbele, ikiwemo huduma za jamii, miundombinu, na miradi ya kukuza uchumi, ambao utaimarisha zaidi uhusiano kati ya nchi zetu na kuongeza uwezo wake wa kuleta manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili,” alisema Dkt. Mwamba.
Kaimu Balozi wa Hungary Nchini, Mhe. David Tòth, akizungumza jambo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (hayupo pichani), katika Ofisi za Wizara ya Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma, ambapo walijadiliana kuimarisha zaidi ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi na Tanzania, hasa kupitia utekelezaji wa miradi ya maji na maendeleo ya kijamii.

Kwa upande wake, Mhe. David Toth, alieleza dhamira ya Serikali ya Hungary ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wake na Tanzania, akisisitiza kuwa mradi wa maji wa Biharamulo ni mfano wa ushirikiano wa kimaendeleo unaolenga kuboresha maisha ya wananchi moja kwa moja.

“Hungary inaiona Tanzania kama mshirika muhimu wa maendeleo barani Afrika, na tumejidhatiti kuunga mkono miradi inayogusa maisha ya wananchi, ikiwemo mradi huu wa maji wa Biharamulo ambao utaongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa Kagera,” alisema Mhe. Toth.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (Katikati), Kaimu Balozi wa Hungary Nchini, Mhe. David Tòth (wa tano kushoto), Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban (wa tano kulia), Kaimu Kamishna wa Idara ya Uchambuzi wa Sera, Dkt. Remidius Ruhinduka (wa tatu kushoto), Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje Wizara ya Fedha, Bw. Rished Bade (wa nne kulia), Kamishna Msaidizi Idara ya Fedha za Nje Wizara ya Fedha, Bw. Melkizedeck Mbise (wa tatu kulia), Kamishna Msaidizi Idara ya Uchambuzi wa Sera, Bw. William Mhoja (kushoto), Mtaalamu wa Miradi ya Maji, Wizara ya Mambo ya Nje na Biashara ya Hungary, Bw. Szabolcs Nagy (wa nne kushoto) na Maafisa wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha, na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kukutana na kufanya mazungumzo, katika Ofisi za Wizara ya Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma, kuhusu kuimarisha zaidi ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na Hungary, hasa kupitia utekelezaji wa miradi ya maji na maendeleo ya kijamii.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma).

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban, Kaimu Kamishna wa Idara ya Uchambuzi wa Sera, Dkt. Remidius Ruhinduka, Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje Wizara ya Fedha, Bw. Rished Bade, Kamishna Msaidizi Idara ya Fedha za Nje Wizara ya Fedha, Bw. Melkizedeck Mbise, Mtaalamu wa Miradi ya Maji, Wizara ya Mambo ya Nje na Biashara ya Hungary, Bw. Szabolcs Nagy na Maafisa wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha, na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here