JESHI la Polisi Mkoa wa Kagera limekanusha taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii zikidai kuwepo kwa mizoga ya ng’ombe wa kisasa iliyokufa au kuuawa kufuatia mgogoro kati ya wakulima na wafugaji mkoani humo.
Kupitia taarifa rasmi kwa umma iliyotolewa leo Januari 16, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera amesema kuwa, hakuna tukio kama hilo lililotokea ndani ya mkoa huo, akibainisha kuwa madai hayo hayana ukweli wowote.
Aidha, Jeshi la Polisi limeeleza kuwa, hakuna ufugaji mkubwa wa ng’ombe wa aina inayodaiwa katika Mkoa wa Kagera, ambapo ufugaji unaotambulika zaidi ni wa ng’ombe wa asili aina ya Ankole.
Jeshi la Polisi limeonya vikali dhidi ya vitendo vya kuunda na kusambaza taarifa za upotoshaji kupitia mitandao ya kijamii kwa lengo la kuchochea taharuki miongoni mwa wananchi, likisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika watakaobainika.
Aidha,wananchi wametakiwa kupuuza taarifa hizo zisizo sahihi na kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia kudumisha amani na utulivu katika mkoa huo.
