NA DIRAMAKINI
JESHI la Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji limewakamata watu wanane wanaodaiwa kuwa waendesha bodaboda kwa tuhuma za kuharibu mali katika Kijiji cha Kiwambo, Kata ya Kitomondo, Tarafa ya Kisiju, wilayani Mkuranga.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji leo Januari 17,2026, tukio hilo lilitokea Januari 16, 2026, majira ya saa 11:30 jioni, wakati watuhumiwa hao walipokuwa wakielekea kumpumzisha bodaboda mwenzao aliyefariki dunia kufuatia ajali ya kugongwa na gari eneo la Keko jijini Dar es Salaam.Inadaiwa kuwa,watuhumiwa walifanya vurugu kwa kuvunja vioo vya mbele vya magari 16 pamoja na mabasi mawili ya kubeba abiria yaliyokuwa yakipita eneo hilo, kwa kutumia mawe na vipande vya tofali, wakidai kulipiza kisasi kwa tukio hilo.
Jeshi la Polisi limethibitisha kuwa pikipiki tatu zilizokuwa zikitumiwa na watuhumiwa wakati wa kutekeleza vitendo hivyo zimekamatwa.
Pikipiki hizo zina namba za usajili MC 574 EQP, MC 496 FJG na pikipiki nyingine yenye chasis namba BX2SWG66853G7, zote aina ya Boxer.
Watuhumiwa kwa sasa wanashikiliwa katika Kituo cha Polisi Mkuranga kwa ajili ya mahojiano zaidi, huku taratibu za kisheria zikiendelea ili kuwafikisha mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji limetoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za wahalifu ili sheria ichukue mkondo wake.
Aidha, Polisi wamesisitiza kuwa hawatasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo vya kihalifu vinavyohatarisha usalama wa raia na mali zao.