Polisi wachunguza kifo cha mtoto Mtwara, wahalifu wakamatwa

NA DIRAMAKINI

JESHI la Polisi Mkoa wa Mtwara linaendelea kuchunguza tukio la kusikitisha la kifo cha mtoto Shaban Muebo (12), mkazi wa Kijiji cha Masyalele, Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara lililotokea Januari 23, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, mtoto huyo alifariki dunia baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa vibaya kwa kutumia kiwembe, baada ya kutekwa na kupelekwa katika msitu wa jando uliopo kijijini hapo. Inadaiwa kuwa mtuhumiwa wa tukio hilo ni Ibrahim Salumu Kelvine (4), mkazi wa kijiji hicho hicho.

Mtuhumiwa alikamatwa mara baada ya tukio hilo, huku uchunguzi wa kina ukiendelea. Wakati huohuo, majeruhi aliyehusika katika tukio hilo anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Misheni Ndanda, Wilaya ya Masasi.

Katika hatua nyingine za kupambana na uhalifu, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Askari wa Wanyamapori wa Pori la Akiba limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili, Ignas Aron Mponzi (37), mwalimu wa shule ya msingi Namitende, na Dickson Ado (46), mkulima, wakazi wa Kijiji cha Nang’umbu, Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.

Watuhumiwa hao walikamatwa kwa kosa la kupatikana na nyara za serikali (meno ya tembo) walipokuwa wakisafiri kwa kutumia pikipiki aina ya TVS isiyo na namba za usajili, wakitoka Wilaya ya Ruangwa kuelekea Wilaya ya Masasi.

Walikamatwa wakiwa katika nyumba ya kulala wageni (jina limehifadhiwa) wakisubiri mnunuzi wa nyara hizo.

Aidha, tarehe Januari 17, 2026, Jeshi la Polisi liliwakamata Abas Mohamed Nakiti (49) na Mohad Mohamed Nakiti (22), wakulima na wakazi wa Kijiji cha Mkachima, Wilaya ya Masasi, wakiwa na jumla ya viroba 10 vya dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa kilogramu 110.

Inadaiwa kuwa dawa hizo zilihifadhiwa nyumbani kwa Abas Mohamed kwa lengo la kujipatia kipato.

Pia, watuhumiwa wengine watatu, Ramadhani Abdallah Said (32), Sharafi Hussein Rajabu (22) na Bashiru Iddi Omary (23), wakazi wa Kijiji cha Mkachima, walikamatwa wakiwa na viroba nane vya bangi yenye uzito wa kilogramu 94, wakituhumiwa kuhifadhi na kusafirisha dawa hizo kwa lengo la biashara haramu.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara limesema linaendelea na operesheni maalumu za kudhibiti uhalifu, ikiwemo kupiga vita vitendo vya ujangili, uuzaji na usambazaji wa dawa za kulevya, ambavyo ni kinyume na sheria za nchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here