Tanga yanufaika na elimu ya fedha, wananchi 5,000+ wafikiwa

TANGA-Zaidi ya wananchi 5,000 wa Mkoa wa Tanga wamepatiwa elimu ya fedha baada ya kushiriki Maadhimisho ya Tano ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yaliyofanyika kuanzia Januari 19 hadi 26, 2026 katika viwanja vya Usagara, jijini Tanga.
Tukio hilo lililolenga kuwawezesha wananchi kutumia huduma rasmi za kifedha kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii limepata mwitikio mkubwa kutoka kwa wajasiriamali, vijana, wanawake, wanafunzi, wavuvi na watumishi wa umma.

Maadhimisho hayo yamefungwa rasmi Januari 26, 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi, Dkt. Batilda Buriani, yakiwa na kauli mbiu: “Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii.”

Akizungumza katika hafla ya kufunga maadhimisho hayo, Dkt. Buriani aliwashukuru wananchi na wadau wa sekta ya fedha kwa kushiriki kwa wingi, akibainisha kwamba elimu waliyoipata itawawezesha kutumia huduma za kifedha rasmi, kuboresha maisha yao na kuchangia ukuaji wa uchumi wa familia na Taifa.
"Maadhimisho haya yamepata mwitikio mkubwa, ambapo wananchi 5,000 wakiwemo wajasiriamali, wanawake, vijana, wavuvi, wanafunzi na watumishi wa umma walipatiwa elimu ya kina kuhusu usimamizi wa fedha binafsi, uwekaji wa akiba, mikopo, uwekezaji, bima na namna ya kusuluhisha migogoro ya kifedha kupitia taasisi rasmi,” alisema Dkt. Buriani.

Aliongeza kuwa maadhimisho hayo yanafanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha.

Akiongea kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Kaimu Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bi. Dionisia Mjema, alisema maadhimisho hayo ni utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa mwaka 2020/21–2029/30, unaolenga kuimarisha ulinzi wa watumiaji wa huduma za fedha na kuongeza ujumuishaji wa kifedha.

Aliongeza kuwa hadi Desemba 2026, elimu ya fedha ilitolewa katika Mikoa 17 na Halmashauri 94, na kuwafikia jumla ya wananchi 64,125, wakiwemo wanaume 22,445 na wanawake 41,680.
"Katika mkoa wa Tanga, jumla ya washiriki 5,350 walifundishwa katika masuala mbalimbali ikiwemo usimamizi wa fedha binafsi, uwekaji wa akiba, mikopo yenye nidhamu, uwekezaji katika masoko ya mitaji na mifuko ya uwekezaji, bima ya afya na maisha, kodi, na maandalizi ya uzeeni,” alisema Bi. Mjema.

Alibainisha kuwa maadhimisho hayo yamewezesha wananchi kuelewa haki na wajibu wao kifedha, na kuhamasishwa kutumia fursa zilizopo katika sekta ya fedha.

Kwa upande wa baadhi ya Washiriki walisema kuwa mafunzo hayo yamewapa uelewa wa kina. Asha Mwinuka, mfanyabiashara mdogo wa Tanga, alisema: “Sasa ninafahamu namna ya kuweka akiba, kuwekeza kwa nidhamu na kufuata masharti ya mikopo. Hii itasaidia biashara yangu na familia yangu kupata mapato zaidi.”

Vilevile, Juma Maulid, mwanafunzi wa Chuo cha Masai Utalii jijini Tanga, alisema kuwa elimu ya bima na uwekaji wa akiba itamuwezesha kujiandaa kwa maisha yake ya baadaye.
Viongozi hao pia waliwashukuru wadau, benki na wadhamini wakiwemo Benki Kuu ya Tanzania, NMB, NBC, Benki ya Biashara ya Mwalimu, UTT-AMIS na PSSSF, kwa mchango wao mkubwa uliowezesha kufanikisha maadhimisho hayo.

Maadhimisho hayo yameleta mafanikio kadhaa kwa wananchi na sekta ya fedha kwa ujumla; yakiwemo, Kwanza, idadi ya watu wenye uelewa wa kifedha imeongezeka, na wananchi wamepata maarifa juu ya upatikanaji na matumizi ya bidhaa na huduma rasmi za kifedha.

Pili, uelewa na matumizi ya masoko ya fedha yameimarika, na huduma za kifedha zimekusudiwa kuwa karibu zaidi na wananchi.
Aidha, maadhimisho yamewezesha wananchi kuelewa haki na wajibu wao, kujifunza namna bora ya kusimamia rasilimali zao, na kuongeza uwezo wa wajasiriamali kuunganisha biashara zao na fursa zinazotolewa na sekta ya fedha. Wananchi na wamejengewa utamaduni wa kutumia huduma rasmi za kifedha, jambo linalochochea ukuaji wa uchumi wa familia, jamii na Taifa kwa ujumla.

Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanatarajiwa kuendelea kufanyika kila mwaka katika mikoa mbalimbali ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya fedha, kukuza uwekezaji na kuongeza ujumuishaji wa kifedha.

Mafanikio haya yanadhihirisha kwamba elimu ya fedha si tu nyenzo ya uelewa wa kifedha, bali pia ni msingi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, sambamba na malengo makuu ya Taifa ya kuongeza Pato la Mtu Mmoja Mmoja na Pato Taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here