ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi, amewataka Waumini wa Dini ya Kiislamu kujipamba na Qurani Tukufu, kuishi kwa kufuata miongozo na mafundisho yake pamoja na kuifanya Qurani kuwa dira ya maisha yao ya kila siku.
Alhaj Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Januari 31, 2026 aliposhiriki Mashindano ya Kimataifa ya Kuhifadhi Qurani, yaliyoandaliwa kwa ushirikiano wa Taasisi ya Al arabiha ya Oman na Afisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, yaliyofanyika katika Msikiti wa Jamiu Zanzibar, Kiembe Samaki, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amewanasihi Waumini wa Dini ya Kiislamu pamoja na Wananchi kwa ujumla kushikamana, kuishi kwa umoja, kusaidiana na kudumisha maadili mema ili kupata baraka za Mwenyezi Mungu.
Halikadhalika, amesisitiza umuhimu wa kuishi kwa kupendana, kuimarisha malezi bora ya vijana pamoja na kulinda amani na utulivu wa nchi, akieleza kuwa misingi hiyo ni nguzo muhimu ya maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza Taasisi ya Al arabiha ya Oman pamoja na Afisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar kwa kufanikisha mashindano hayo, pamoja na mchango wao mkubwa katika kuihudumia jamii kupitia sekta za elimu, afya, chakula na huduma za kijamii kupitia kambi mbalimbali.
Amesisitiza umuhimu wa kuendeleza na kuimarisha ushirikiano kati ya Taasisi hizo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Vilevile, Rais Dkt. Mwinyi amewapongeza washiriki wa mashindano hayo na kuwahimiza kuendelea kushikamana na Qurani Tukufu sambamba na taaluma walizonazo ili kufanikisha mafanikio zaidi duniani na Akhera.
Mashindano hayo ya Kimataifa yamehusisha washiriki sita kutoka nchi za Ujerumani, Uganda, Tanzania, Urusi, Canada na Brazil, ambapo mshiriki Ndg. Usama Barghouth kutoka Ujerumani ameibuka mshindi wa kwanza na kutunukiwa kombe, cheti pamoja na zawadi ya shilingi milioni 20.

















