Salamu za Jumapili:Omba simamisha jua

NA LWAGA MWAMBANDE

MAOMBI ni nguzo muhimu ya imani ya Kikristo na njia kuu ya mawasiliano kati ya Mkristo na Mungu. Kupitia maombi, Mkristo huimarisha uhusiano wake wa kiroho na hupata nguvu na amani ya moyo.
Rejea katika neno la Mungu,kitabu cha Yeremia 29:12-14..."nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza. Nanyi mtanitafuta na kuniona,mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.Nami nitaonekana kwenu asema BWANA."

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, maombi humsaidia Mkristo kustahimili changamoto za maisha, kupunguza wasiwasi na kuimarisha maamuzi yenye busara. Aidha, humjenga kimaadili kwa kukuza upendo,uvumilivu na unyenyekevu.

Kwa ujumla, maombi humwezesha Mkristo kuishi maisha yenye matumaini, mwelekeo na amani ya ndani.Endelea;

1. Omba maombi ya nguvu, umweleze Mungu wako,
Ukiwa na utulivu, asikia Mungu wako,
Yahitaji ushupavu, na tena Imani yako,
Yoshua limwomba Mungu, akasimamisha jua.

2. Walikuwa wapigana, nao Waamori huko,
Na Yoshua akaona, ushindi ulikuweko,
Ila giza aliona, litafanya usiweko,
Yoshua limwomba Mungu, akasimamisha jua.

3. Kwa ile Imani yake, na ule wake upako,
Lishusha maombi yake, jua lizidi kuweko,
Limgusa Mungu wake, mwanga ukazidi weko,
Yoshua limwomba Mungu, akasimamisha jua.

4. Ushindi waloutaka, nao huo ukaweko,
Ndiye Mungu mtukuka, aliyewajibu huko,
Yale yaliyofanyika, leo yaweza kuweko,
Yoshua limwomba Mungu, akasimamisha jua.

5. Lipi linalokusibu, wataka majibu yako,
Omba si kwa kujaribu, kumaanisha kuweko,
Mungu wako atajibu, hata kukupa kicheko,
Yoshua limwomba Mungu, akasimamisha jua.

6. Mungu wa yule Yoshua, huyo ndiye ni wa kwako,
Alisimamisha jua, na ushindi ukaweko,
Omba simamisha jua, amani kwako iweko,
Yoshua limwomba Mungu, akasimamisha jua.

7. Livyofanya kwa Yoshua, aweza kufanya kwako,
Hili ukishalijua, liwe ujasiri kwako,
Likushikalo amua, shusha kwa Mungu si lako,
Yoshua limwomba Mungu, akasimamisha jua.

8. Atasimamisha jua, yote kwa ajili yako,
Kwa vile anatambua, hayo mahitaji yako,
Ambaye umeibua, mkono wake uweko,
Yoshua limwomba Mungu, akasimamisha jua.

9. Twashukuru Mungu wetu, ulikuweko na uko,
Hata zote shida zetu, twaweza zileta kwako,
Hata zile ngumu kwetu, zinatatulika kwako,
Yoshua limwomba Mungu, akasimamisha jua.

10. Mungu simamisha jua, ili ushindi uweko,
Yatutingayo tatua, ili amani iweko,
Wewe peke tunajua, hayashindikani kwako,
Yoshua limwomba Mungu, akasimamisha jua.
(Yoshua 10:12)

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here