DODOMA-Serikali imeweka afua madhubuti ya kutoa elimu ya malezi kwa akina mama wanaporudi nyumbani baada ya kujifungua, kwa lengo la kupunguza vifo vya watoto wachanga vinavyotokea majumbani pamoja na kudhibiti tatizo la watoto kuzaliwa kabla ya muda.
Akijibu swali la nyongeza, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Florence Samizi amesema Serikali imeandaa muongozo maalum wa elimu ya afya kwa akina mama wanaojifungua, unaoendelea kutolewa kupitia watoa huduma za afya ngazi ya jamii.
Dkt. Samizi amesema miongoni mwa elimu inayotolewa ni umuhimu wa kumpatia mtoto joto kwa kutumia njia ya Kangaroo Mother Care, hususan kwa watoto wachanga njiti, ili kusaidia ukuaji wao na kupunguza hatari ya maambukizi.
Ameongeza kuwa akina mama wanaelimishwa kuhusu unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee, akisisitiza kuwa maziwa ya mama yana faida kubwa kiafya zaidi ya chakula, ikiwemo kuongeza kinga ya mwili kwa mtoto na kusaidia ukuaji bora.
Aidha, Dkt. Samizi amesema elimu nyingine muhimu inayotolewa ni kuhusu chanjo za mtoto, ili kumkinga dhidi ya magonjwa mbalimbali, pamoja na kumpa mama ratiba ya kliniki na kusisitiza umuhimu wa kuhudhuria kliniki kwa wakati.
Vilevile, amebainisha kuwa akina mama wanaelimishwa kuhusu dalili hatarishi kwa mama na mtoto, ili waweze kuchukua hatua za haraka na kuwahi kituo cha afya endapo changamoto zitajitokeza.
Dkt. Samizi amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha utoaji wa elimu ya malezi kwa akina mama wakiwa majumbani, kupitia vituo vya afya na wahudumu wa afya ngazi ya jamii, ili kuhakikisha watoto wanapata uangalizi bora na kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika.
