DODOMA-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe ameridhishwa na maandalizi ya mapokezi ya wanafunzi wa darasa la awali na la kwanza katika Shule ya Msingi Iyumbu jijini Dodoma, na kuuarifu umma kuwa maandalizi katika shule zote za msingi 18,055 yamekamilika na zipo tayari kupokea wanafunzi kuanzia Januari 13, 2026.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe akizungumza na walimu wa Shule ya Msingi Iyumbu na viongozi wa mkoa wa Dodoma jana jioni, kuhusu maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wanaotarajiwa kuanza darasa la awali na la kwanza mara baada ya kujiridhisha na maandalizi yaliyofanywa katika shule hiyo ya Msingi Iyumbu.
Prof. Shemdoe amesema, ameitembelea shule hiyo ya Msingi Iyumbu tarehe 12 Januari, 2026, ili kujiridhisha na maandalizi ya mapokezi ya wanafunzi wanaotarajiwa kuanza darasa la awali na la kwanza Januari 13, 2026 na amejionea mwenyewe kuwa maandalizi yamekamilika.
“Tumeona maandalizi kwenye shule hii yamekamilika, kama ilivyo kwenye shule zote 18055 za msingi, hivyo natoa wito kwa wazazi wenye watoto walio na umri wa kuanza darasa la awali na la kwanza wawapeleke shuleni,” Prof. Shemdoe amesisitiza.
Mwonekano wa moja ya darasa la awali lililopo katika Shule ya Msingi Iyumbu, darasa ambalo limeandaliwa kwa ajili ya kuwahudumia wanafunzi wanaoanza darasa la awali leo Januari 13, 2026.Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe akifanya ukaguzi katika moja ya darasa la awali lililopo Shule ya Msingi Iyumbu, ikiwa ni hatua ya kujiridhisha na maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wanaotarajiwa kuanza darasa la awali na la kwanza katika shule hiyo.
Baadhi ya walimu wa Shule ya Msingi Iyumbu wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe alipowasili katika Shule ya Msingi Iyumbu jana jioni, kwa ajili ya ukaguzi wa maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wanaotarajiwa kuanza darasa la awali na la kwanza katika shule hiyo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe akiingia katika moja ya darasa la awali lililopo Shule ya Msingi Iyumbu, ikiwa ni sehemu ya ukaguzi wa maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wanaotarajiwa kuanza darasa la awali na la kwanza katika shule hiyo.Prof. Shemdoe amejionea m6adarasa ya awali mazuri ambayo yamejengwa kwa fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, na kuzielekeza halmashauri zote nchini kutumia mapato ya ndani kujenga miundombinu bora ya elimu kama ambavyo Halmashauri ya Jiji la Dodoma imejenga katika Shule ya Msingi Iyumbu.
Aidha, Prof. Shemdoe amewataka walimu nchini kuhakikisha shule zinatoa wanafunzi wenye ufaulu mzuri kwani Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu, hivyo ufaulu wa wanafunzi ni faraja kwa Mheshimiwa Rais.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema kwamba tangu Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani ufaulu umeongezeka, na kuongeza kuwa sababu kubwa ya kuongezeka kwa ufaulu huo ni uwekezaji fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu ya elimu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe akiwasili katika Shule ya Msingi Iyumbu jana jioni iliyopo jijini Dodoma, kwa ajili ya ukaguzi wa maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wanaotarajiwa kuanza darasa la awali na la kwanza katika shule hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akisisitiza jambo kwa Prof. Shemdoe kuhusu maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wanaotarajiwa kuanza darasa la awali na la kwanza, yaliyofanywa na uongozi wa Shule ya Msingi Iyumbu jijini Dodoma.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Iyumbu, Bi. Monica Nshimba akimuongoza Prof. Shemdoe kukagua miundombinu ya shule yake, ambayo imeandaliwa kwa ajili kuwapokea wanafunzi wanaotarajiwa kuanza darasa la awali na la kwanza katika shule hiyo.Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Iyumbu, Bi. Monica Nshimba amemshukuru Prof. Shemdoe kwa kuitembelea shule yake na kumuahidi kwamba walimu wako tayari kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kutimiza lengo la Serikali la kutoa elimu bora ya msingi kwa wananchi wake.
Naye, Diwani wa Kata ya Iyumbu Mhe. Sadiki Mponyamili amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia kata yake fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha Shule ya Msingi Iyumbu na ameipatia kata yake zaidi ya Shilingi Milioni 150 kwa ajili ya kuboresha shule ya Sekondari.


