DODOMA-Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Rajabu Mabele amewataarifu vijana wote wa Tanzania Bara na Visiwani kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa kujitolea kwa mwaka 2026.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na Kurugenzi ya Habari na Uhasiano, Makao Makuu ya JKT, utaratibu wa kuomba na kuchaguliwa kujiunga na mafunzo hayo unaratibiwa na ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wilaya kulingana na eneo anakoishi mwombaji.
Usajili wa kujiunga na mafunzo hayo utaanza rasmi tarehe 26 Januari 2026 katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani.
"Vijana watakaoteuliwa kujiunga na mafunzo hayo watatakiwa kuripoti katika makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa kuanzia Februari 27 hadi Machi 04, 2026,"imeeleza taarifa hiyo.
Aidha, Jeshi la Kujenga Taifa limewataka vijana watakaopata fursa hiyo kufahamu kuwa halitoi ajira wala halihusiki na kuwatafutia ajira katika asasi, vyombo vya ulinzi na usalama au mashirika ya serikali na binafsi. Badala yake, JKT hutoa mafunzo yatakayowawezesha vijana kujiajiri wenyewe mara baada ya kumaliza mkataba wao wa mafunzo.
Taarifa zaidi kuhusu sifa za waombaji pamoja na maelekezo ya vifaa vinavyopaswa kuzingatiwa wakati wa kuripoti makambini zinapatikana kupitia tovuti rasmi ya Jeshi la Kujenga Taifa ambayo ni www.jkt.mil.com.
