NA DIRAMAKINI
LIGI Kuu ya NBC Tanzania Bara msimu wa 2025/2026 inaendelea kushika kasi huku ushindani mkali ukishuhudiwa katika nafasi za juu, kati na chini ya msimamo wa ligi hiyo.
Aidha,kwa sasa, timu ya JKT Tanzania inaongoza msimamo wa ligi baada ya kucheza michezo 11, ikikusanya pointi 20 kufuatia ushindi mara tano, sare tano na kipigo kimoja.
Katika nafasi ya pili ni Young Africans SC, ambayo imeonesha ubora mkubwa kwa kucheza michezo saba pekee, kushinda sita na sare moja, bila kupoteza mchezo wowote.
Yanga SC imejikusanyia pointi 19 na tofauti ya mabao 17, ikiwa ni miongoni mwa timu zenye safu bora ya ushambuliaji.
Nafasi ya tatu inashikiliwa na Pamba Jiji, yenye pointi 16, ikifuatiwa na Simba SC katika nafasi ya nne ikiwa na pointi 13, sawa na Azam FC iliyopo nafasi ya tano.
Simba imecheza michezo sita pekee, hali inayoipa nafasi nzuri ya kupanda juu zaidi endapo itaendelea kufanya vizuri katika michezo ijayo.
Katikati ya msimamo, timu kama Mashujaa FC, Namungo FC na Mtibwa Sugar zinaendelea kupambana kusogea juu, huku tofauti ya pointi ikiwa ndogo kati ya timu hizo. Mashujaa FC licha ya kuwa na pointi 13, inakabiliwa na changamoto ya kuruhusu mabao mengi.
Kwa upande wa chini ya msimamo, Mbeya City, Tanzania Prisons na Dodoma Jiji zinaendelea kusaka matokeo chanya ili kujinasua katika mstari wa hatari.
Vilevile, KMC FC inashika mkia wa ligi ikiwa na pointi nne pekee baada ya michezo tisa, hali inayoiweka katika nafasi mbaya zaidi.
