Vyuo mbalimbali Tanga kushiriki utalii wa kimasomo Wiki ya Huduma za Fedha

TANGA-Vyuo mbalimbali jijini Tanga vimeonesha utayari wa kushiriki kikamilifu katika mafunzo ya elimu ya fedha yatakayotolewa wakati wa Wiki ya Huduma ya Fedha kitaifa, itakayofanyika katika viwanja vya Usagara, jijini Tanga.
Hayo yamesemwa kwa nyakati tofauti na Viongozi wa baadhi ya vyuo vya elimu ya juu vilivyoko mjini Tanga walipotembelewa na Timu ya Wataalam wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, ambapo Mkurugenzi wa Chuo cha Uhasibu Tanga (TIA), Dkt. Mwita Sospeter Mkami, alisema elimu ya fedha ni muhimu kwa wanafunzi kutokana na changamoto za usimamizi wa fedha wanazokumbana nazo, hususan wanaopokea mikopo na fedha za matumizi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Tanga, Bw. Gideon Ole Lairumbe, aliishukuru Serikali kwa kuuchagua Mkoa wa Tanga kufanyika maadhimisho hayo, akisema ni fursa muhimu kwa wakufunzi na wanafunzi kuongeza uelewa wa masuala ya fedha na kujiandaa kiuchumi.
Akizungumzia kuhusu ziara hiyo Mchumi Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bw. Thobias Kanyoki, kwa niaba ya Timu ya Wizara ya Fedha, baada ya kutembelea vyuo hivyo alisema kuwa malengo ya ziara hiyo lilikuwa kuwaaalika wakufunzi, wanafunzi na watumishi kushiriki mafunzo hayo kama sehemu ya utalii wa kimasomo.

Vile vile, wawakilishi wa Wizara ya Fedha walisema elimu ya fedha inalenga kuimarisha uwezo wa wananchi katika kupanga matumizi, kuweka akiba na kutumia fursa za kiuchumi, sambamba na utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Elimu ya Fedha na mitaala mipya mashuleni.
Katika ziara hiyo, Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ilitembelea vyuo vinne, vikiwemo Chuo cha Utumishi wa Umma Tanga, Chuo cha Uhasibu TIA Tanga, Chuo cha Masai Utalii na Chuo cha Ufundi Stadi VETA Tanga.

Wiki ya Huduma za Fedha itahusisha ushiriki wa taasisi mbalimbali za fedha ikiwemo mabenki, taasisi za bima,masoko ya mitaji, taasisi za mikopo midogo na wadau wengine wa sekta ya fedha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here