Yoweri Museveni ashinda tena urais Uganda, upinzani wakataa matokeo

KAMPALA-Tume ya Uchaguzi ya Uganda imemtangaza Rais Yoweri Kaguta Museveni kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika Alhamisi ya wiki hii, hatua inayomruhusu kuendelea kushika hatamu za uongozi kwa kipindi kingine cha miaka mitano na hivyo kurefusha utawala wake hadi kufikia zaidi ya miongo minne tangu aingie madarakani.
Kwa mujibu wa matokeo rasmi yaliyotolewa na Tume hiyo, Museveni alipata asilimia 72 ya kura zote zilizohesabiwa, akimshinda kwa tofauti kubwa mpinzani wake wa karibu, mwanasiasa wa upinzani na mwanamuziki Robert Kyagulanyi Ssentamu maarufu Bobi Wine, aliyepata asilimia 25 ya kura.

Matokeo hayo yanaashiria ushindi wa saba mfululizo kwa Museveni tangu aingie madarakani mwaka 1986.

Hata hivyo, mara baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Bobi Wine aliyapinga vikali akidai kuwa hayakuwa halali.

Kupitia taarifa yake kwa umma, aliyatuhumu matokeo hayo kuwa ya kughushi na kudai kuwa kulikuwapo vitendo vya kujazwa kura bandia katika vituo kadhaa vya kupigia kura.

Licha ya madai hayo mazito, Wine hajawasilisha ushahidi wa wazi unaothibitisha tuhuma zake, huku mamlaka husika, ikiwemo Tume ya Uchaguzi na vyombo vya usalama, bado hazijatoa majibu ya kina kuhusu tuhuma hizo.

Katika hatua nyingine, kiongozi huyo wa upinzani amewataka wananchi wa Uganda kuandamana kwa amani ili kupinga matokeo hayo, akisisitiza umuhimu wa kulinda haki ya raia kuchagua viongozi wao kwa misingi ya uwazi na haki.

Wito huo umeibua mjadala mpana ndani na nje ya Uganda kuhusu mustakabali wa demokrasia na uhuru wa kisiasa nchini humo.

Rais Museveni, mwenye umri wa miaka 81, aliingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 1986 baada ya kuongoza harakati za waasi zilizopindua serikali ya wakati huo.

Tangu hapo, amekuwa mhimili mkuu wa siasa za Uganda, akijenga utawala mrefu ambao umeleta mafanikio kadhaa ya kiuchumi na kiusalama, lakini pia umekosolewa kwa madai ya kubana nafasi ya upinzani na uhuru wa kisiasa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here