MOROGORO-Wajumbe tisa wa Kamati Elekezi ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Wizara ya Fedha wameanza mafunzo maalum ya ufuatiliaji na tathmini yenye lengo la kuwaongezea uwezo katika matumizi ya mbinu bora za ufuatiliaji na tathmini na kuratibu shughuli za ufuatiliaji na tathmini kwa ufanisi.
Mafunzo hayo, yanayoratibiwa na Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini cha Wizara ya Fedha, yanafanyika kwa muda wa siku mbili katika ukumbi wa mikutano wa Cate Hotels, Morogoro, na yanatolewa na wawezeshaji kutoka Kituo cha Umahiri katika Ufuatiliaji na Tathmini, Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Kamati Elekezi ya Ufuatiliaji na Tathmini ni chombo muhimu kinachosimamia na kuimarisha utekelezaji wa shughuli za ufuatiliaji na tathmini.Hivyo, Kamati hii ina jukumu la kumshauri Katibu Mkuu kuhusu hatua za kimkakati zinazopaswa kutekelezwa kwa kuzingatia taarifa za ufuatiliaji na tathmini katika kuboresha uwajibikaji na utendaji wa Wizara na taasisi zilizo chini yake.
Aidha, Kamati Elekezi ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Wizara ya Fedha inatarajiwa kuzinduliwa rasmi siku ya Jumamosi, tarehe 24 Januari 2026, na Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bw. Lusius Mwenda.




