Wizara ya Fedha yaendelea kutoa elimu ya fedha kwa makundi mbalimbali jijini Tanga

TANGA-Wizara ya Fedha kupitia Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha imeendelea kutoa elimu ya fedha kwa makundi mbalimbali ya jamii mkoani Tanga, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha yanayoendelea katika Viwanja vya Usagara, jijini Tanga, kwa lengo la kuwajengea wananchi uelewa wa masuala ya kifedha na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.
Akizungumza wakati wa utoaji wa elimu katika darasa la Elimu ya Fedha, Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bi. Grace Muiyaza, alisema mafunzo hayo yanawalenga watumishi wa umma, wafanyabiashara wadogo, vikundi vya wajasiriamali, wananchi wa kawaida pamoja na wanafunzi kuanzia ngazi ya shule ya msingi, sekondari hadi vyuoni.

“Tuko hapa tunatoa mafunzo kwa makundi yote ya jamii ya Tanga. Lengo letu ni kuwajengea uelewa wa masuala ya kifedha na kuwawezesha kushiriki vizuri katika shughuli za kiuchumi,” alisema Bi. Muiyaza.
Alieleza kuwa katika darasa la siku hiyo, walikutana na wanafunzi wa Shule ya Msingi Usagara na kuwapatia elimu ya usimamizi wa fedha binafsi, akisisitiza kuwa elimu hiyo ni muhimu kwa watoto kwa kuwa nao hupata fedha kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo kwa wazazi wao.

“Watoto nao wanapata fedha kwa matumizi yao ya kila siku, hivyo ni muhimu wafundishwe mapema namna ya kusimamia fedha ili waweze kufikia malengo yao ya muda mfupi na mrefu,” aliongeza.

Bi. Muiyaza alisema darasa hilo lilikuwa shirikishi na wanafunzi walionesha uelewa mzuri kuhusu masuala ya msingi ya usimamizi wa fedha, hususan umuhimu wa kuweka akiba.
Alibainisha kuwa baadhi ya wanafunzi hupatiwa fedha nyingi zaidi ya mahitaji yao ya shule, hali inayowapa fursa ya kuanza utamaduni wa kujiwekea akiba mapema.

Katika hatua nyingine, alitoa wito kwa wazazi na walezi kuwalea watoto wao katika misingi sahihi ya kifedha, ikiwemo kutumia mifumo salama ya kutunza akiba badala ya njia zisizo salama kama vibubu au kuhifadhi fedha chini ya vitanda.

“Bado tunakutana na changamoto kubwa ya watu kuweka fedha kwenye sehemu zisizo salama na rasmi. Tunawahamasisha wazazi na jamii kwa ujumla kutumia benki, vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha, huduma za fedha kwa njia ya simu na kampuni za uwekezaji,” alisema.
Kwa upande wake, mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Usagara, Salma Rajabu, alisema elimu aliyopata imemfungua macho kuhusu umuhimu wa kuweka akiba na kuhifadhi fedha sehemu salama.

“Hapo awali nilijua fedha zinawekwa kwenye kibubu au chini ya kitanda, lakini sasa nimejifunza kuwa ni salama zaidi kuweka benki au kwenye simu. Nitawaelimisha wazazi wangu na kuwaomba wanifungulie akaunti ya akiba,” alisema Salma.

Naye Hassan Mohamed, mwanafunzi wa darasa la sita katika shule hiyo, alisema somo hilo limemsaidia kuelewa umuhimu wa akiba kwa maisha ya baadaye na namna ya kuwashauri wazazi wao kutumia njia salama za kuhifadhi fedha.
Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha yanaendelea mkoani Tanga, yakilenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu huduma za fedha na kuimarisha ujumuishaji wa kifedha kwa makundi yote ya jamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here