MTWARA-Wamiliki wa mabasi ya shule wametakiwa kuwasikiliza madereva wao kwa kuwa madereva ndio wanaoshinda muda mwingi na magari hayo na kufahamu changamoto za magari kuliko wamiliki.
Hayo yamesemwa Januari 6,2026 huko Nandope na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mtwara Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Emilian Kamuhanda wakati wa ukaguzi wa mabasi ya shule sambamba na kutoa elimu kwa madereva na wasimamizi wa wanafunzi.
Pia wamiliki wa mabasi hayo wametakiwa kutambua kwamba wazazi wanalipa ada ya usafiri kwa watoto wao ili kuhakikisha watoto wanasafiri kwa usalama.
Zoezi hili la Ukaguzi wa mabasi yanayobeba wanafunzi ni endelevu ili kuhakikisha magari hayo yanakuwa yamekidhi vigezo vya kusafirisha wanafunzi sambamba na kukagua leseni za madereva kama bado wana sifa ya kuendelea kuendesha magari hayo.Jumla ya magari 17 yalikaguliwa Manispaa ya Mtwara Mikindani kati ya hayo magari matano yalikutwa na changamoto mbalimbali kwenye mifumo ya breki na usukani wamiliki wametakiwa kurekebisha kasoro hizo ili magari hayo yaweze kukaguliwa tena na mtaalamu wa mifumo ya vyombo vya moto.
ACP Kamuhanda ametoa wito kwa wazazi na walezi kuendelea kufuatilia kwa karibu juu ya hali ya usafiri wanaotumia watoto kwenda na kurudi shuleni.

