Waziri Kombo aweka jiwe la msingi ujenzi wa jengo la mafunzo kwa watumishi wa umma

ZANZIBAR-Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb) ameweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa Jengo la mafunzo kwa watumishi wa Umma katika Chuo cha Utawala wa Umma (IPA) Zanzibar ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa jengo la mafunzo kwa watumishi wa umma Tunguu - Zanzibar, Waziri Kombo ametoa rai kwa walimu na wanafunzi wa chuo hicho kujiendeleza zaidi ili taaluma zao ziwiane na mahitaji ya sasa.

Balozi Kombo amesema katika dunia ya sasa yenye mabadiliko makubwa ya teknolojia, lazima watumishi wa umma waongeze maarifa ili wasiachwe nyuma wakati wengine wanakimbia.
Waziri Kombo amesema,chuo hicho kinapaswa kujumuisha masomo yanayohusu matumizi ya TEHAMA akitoa mfano namna akili unde (AI) inavyoweza kutumika kuwaundia watu picha na sauti kama kwamba wanafanya kitu husika.

“Maendeleo si uzuri wa jengo pekee, bali maudhui ndiyo yanayohitajika katika kuwajenga wanafunzi kwenda na mabadiliko kwa kutambua dunia inahitaji nini na kwa wakati gani,”alisema.

Aidha, amesema katika mafunzo ya itifaki na diplomasia, wanafunzi wajitahidi kujifunza vyema namna ya kukabiliana na viongozi wa ngazi mbalimbali duniani, kujiamini na kuwa na weledi wanapopandishwa majukwaani kuzungumza masuala yanayohusu mahusiano ya kimataifa.

Ameipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya Mheshimiwa Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa jitihada kubwa inazochukua kuleta maendeleo katika sekta mbalimbali hali inayoonesha dhamira ya kuipaisha nchi.
Amesema, kwa upande wa Muungano, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amekuwa mfano wa viongozi wanaoheshimika duniani kwa namna anavyotumia rasilimali za nchi kwa maslahi mapana ya Watanzania.

Waziri Kombo ameahidi kuwapatia wanafunzi na walimu wa chuo hicho nafasi za elimu ya juu kupitia Jamhuri ya Muungano na akianza na nafasi tano ambapo alisema watakaonufaika ni wale walioomba na kukubaliwa vyuoni.

Mapema, Mkuu wa chuo hicho Dkt. Shaaban Mwinchumu Suleiman, alisema IPA imekuwa ikikodi kumbi za taasisi nyengine kusomeshea watumishi hivyo Serikali ,Bodi na Uongozi wa chuo umeona iko haja kuwa na jengo lake ambalo ni la kisasa ili kuepusha gharama.
"Ujenzi huu ambao ni sehemu ya matunda ya Mapinduzi, utakuwa suluhisho la sehemu za kutoa mafunzo kwa viongozi watumishi wa serikali na taasisi binafsi, na mazingira mazuri ya kujifunza na kufundishia,” alieleza Dkt. Mwinchum.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here