DAR-Mjumbe wa Kamati ya Kisiasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Wang Yi, anatarajiwa kufanya ziara rasmi hapa nchini tarehe 9 na 10 Januari 2026.

Akiwa nchini Mheshimiwa Wang Yi atapokelewa na mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.).
Vilevile, Mhe. Wang Yi anatarajiwa kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ziara hii mbali na kuendelea kuimarisha na kudumisha uhusiano na ushirikiano wa kimkakati uliopo kati ya Tanzania na China, pia inalenga kufuatilia na kuanza utekelezaji wa makubaliano mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo mpango kazi uliopitishwa wakati wa mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (Forum on China-Africa Cooperation -FOCAC), uliofanyika Beijing, China, Septemba 2024.
Tanzania na China zimekuwa zikishirikiana katika maeneo mbalimbali ikiwemo biashara na uwekezaji, ambapo kwa mwaka 2024 thamani ya biashara kati ya Tanzania na China ilifikia takriban dola za Marekani bilioni 5.2.
Kampuni za China pia zimeendelea kuwekeza nchini katika sekta za viwanda, kilimo, huduma, usafirishaji, mawasiliano na utalii. Kwa mwaka 2025, Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) ilisajili miradi ya China 343 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 3.1 na kuzalisha ajira 82,404.
Tanzania na China pia zimekuwa zikishirikiana katika sekta ya miundombinu ya uchukuzi ambapo reli ya TAZARA ni moja wapo ya alama ya urafiki na ushirikiano kati ya nchi hizi mbili.
Reli hiyo ina urefu wa kilomita 1860 ambapo, kilomita 975 zipo Tanzania na kiliomita 885 zipo Zambia, na imebaki kuwa kielelezo cha kihistoria cha uhusiano wa karibu uliojengwa kwa misingi ya umoja, mshikamano na udugu kati ya Tanzania na China.
Aidha, ziara hii ni kielelezo cha uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na China ambao umejengwa kwenye misingi ya kuaminiana na kuheshimiana ukiwa umedumu kwa zaidi ya miongo sita.
Msingi wa ushirikiano huo uliwekwa na waasisi wa mataifa haya, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Mwenyekiti Mao Zedong, ambao unaendelea kuenziwa kwa vitendo na viongozi wa mataifa haya.
