Zanzibar ina mchango mkubwa katika maendeleo ya fasihi na utamaduni-Mama Mariam Mwinyi

SHARJAH-Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Mama Mariam Hussein Mwinyi amesisitiza kuwa,Zanzibar ina mchango mkubwa katika maendeleo ya fasihi na utamaduni kutokana na historia yake kama kitovu cha mwingiliano wa tamaduni kupitia biashara ya upepo wa monsuni uliounganisha Afrika, Uarabuni, Bara Hindi na Mashariki ya Mbali.
Ameongeza kuwa, Mji Mkongwe wa Zanzibar, uliotambuliwa kimataifa kama Urithi wa Dunia wa UNESCO, unaendeleza dhana ya “Urithi Hai” unaoishi katika maisha ya kila siku ya wananchi.
Mama Mariam Mwinyi ameyasema hayo Januari 14,2025 wakati aliposhiriki akiwa Mgeni Rasmi katika Tamasha la Fasihi na Kazi za Sanaa za Afrika 2026 (Sharjah Festival of African Literature – SFAL), linalofanyika katika jiji la Sharjah, Umoja wa Falme za Kiarabu tarehe 14 Januari, 2026.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa tamasha hilo, Mama Mariam Mwinyi ameipongeza Sharjah Book Authority chini ya uongozi wa Sheikha Bodour Bint Sultan Al Qasimi kwa kuandaa jukwaa muhimu linaloimarisha ushirikiano wa kitamaduni kati ya Afrika na Ulimwengu wa Kiarabu, hususan katika ukanda wa Bahari ya Hindi.
Aidha, alieleza dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ya kuendelea kulinda na kuendeleza urithi na utamaduni kama msingi wa utambulisho wa taifa, utalii endelevu na maendeleo jumuishi.

Kupitia Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Mama Mariam Mwinyi alibainisha kuwa utamaduni na urithi si historia pekee bali ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya baadaye.

Alitaja kilimo cha mwani kama mfano hai wa urithi usiogusika unaowezesha wanawake na vijana wa pwani, ambapo zaidi ya wanawake na vijana 1,200 kutoka Unguja na Pemba wamenufaika kupitia programu za kuongeza thamani, kujenga uwezo na kuboresha masoko.
Katika tamasha hilo, Zanzibar imewakilishwa na ujumbe maalum wa ZMBF pamoja na wasanii na wabunifu waliwasilisha kazi mbalimbali za sanaa za mikono, uchongaji wa milango ya Kizanzibari, uandishi wa vitabu, usimulizi wa hadithi za kale, wachoraji na wabunifu wa mavazi ya kitamaduni ya Kiswahili, hatua iliyosaidia kuitangaza Zanzibar kimataifa.

Akihitimisha hotuba yake, Mama Mariam Mwinyi aliwahimiza waandishi, wasanii na wachapishaji wa Afrika kuendelea kusimulia hadithi zao kwa uhalisia, ujasiri na ubunifu, akisisitiza kuwa fasihi na utamaduni ni nyenzo muhimu katika kuunganisha watu, kukuza uelewano na kujenga mustakabali endelevu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here