DAR-Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limethibitisha kuwa msimamo wake ni kwamba michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) itafanyika katika mataifa ya Tanzania, Kenya na Uganda mwaka 2027.
Akizungumza na waandishi wa habari Februari 13, 2026, jijini Dar es Salaam, Rais wa CAF, Dkt. Patrice Motsepe, amesema kwamba uvumi unaosambazwa mitandaoni kuwa mataifa hayo hayako tayari kuandaa mashindano hayo hauna ukweli.
Amesisitiza kuwa AFCON 2027 itakuwa na mafanikio makubwa zaidi katika historia. Dkt.Motsepe ameongeza kuwa,Tanzania, Kenya na Uganda zilijipambanua vizuri kwenye michuano ya CHAN, hivyo hakuna sababu ya kupokonywa nafasi ya kuwa wenyeji wa AFCON 2027.
“Nimeona baadhi ya vyombo vya habari vikidai kuwa nimekuja Tanzania kusema hawataandaa AFCON 2027. Huo ni uongo. Nina imani na mataifa haya na ninajivunia kazi inayofanywa na viongozi wa mpira wa miguu katika mataifa haya matatu,” amesema Dkt. Motsepe.
Aidha, amewataka viongozi wa mataifa hayo kuendelea kushughulikia changamoto za miundombinu ili kuhakikisha mashindano yanafanyika bila kasoro.
