TABORA-Jeshi la Polisi kupitia Kitengo cha Usalama Barabarani wametoa elimu maalum ya usalama barabarani kwa wanafunzi na walimu wa Shule ya Msingi Ilolanguru iliyopo Wilaya ya Uyui, kwa lengo la kuwajengea uelewa sahihi kuhusu matumizi salama ya barabara na kupunguza ajali.
Elimu hiyo ilitolewa na SGT Amran pamoja na CPL David, ambapo waliwafundisha wanafunzi kwa njia ya nadharia na vitendo namna bora ya kutumia barabara kwa usalama.
Katika mada zilizowasilishwa, wanafunzi walielekezwa jinsi sahihi ya kuvuka barabara kwa kutumia kivuko maalum cha watembea kwa miguu (Zebra Cross), pamoja na umuhimu wa kutazama kulia na kushoto kabla ya kuvuka ili kujiridhisha kuwa hakuna hatari.
Aidha, walifundishwa upande sahihi wa kutembea barabarani, kuvuka barabara kwa makundi au mtu mmoja mmoja kwa tahadhari, na kuacha kabisa tabia ya kucheza barabarani ambayo ni hatari kwa maisha yao.
Maafisa hao pia walitoa elimu kuhusu alama mbalimbali za barabarani na matumizi yake, wakisisitiza umuhimu wa kuzitambua na kuzifuata ili kuepusha ajali.



