NA DIRAMAKINI
SERIKALI ya Afrika Kusini imetangaza utayari wa kuandaa Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (2026 Women’s Africa Cup of Nations-WAFCON) ikichukua nafasi ya Morocco ikiwa ni wiki kadhaa zimesalia kabla ya mashindano hayo kuanza.
Hayo yamethibitishwa na Naibu Waziri wa Michezo, Sanaa na Utamaduni wa Afrika Kusini, Mheshimiwa Peace Mabe katika taarifa iliyorushwa na idhaa ya Taifa, akibainisha utayari wa Taifa hilo kusimamia mashindano hayo baada ya Morocco kusita kuendelea nayo.
“Tunaichukua fursa hii ambayo imejileta yenyewe kwa sababu tuna miundombinu hitajika na ushirikiano wa kutosha. Morocco waliposema hawapo tayari kuyaandaa mashindano hayo, sisi Afrika Kusini tukasema tupo tayari kwa mashindano hayo."
Mashindano hayo yanatarajiwa kuanza Machi 17 hadi Aprili 3, mwaka huu ambapo kwa sasa yanaweza kuahirishwa kwa wiki mbili mbele ili kuipa Afrika Kusini nafasi zaidi ya kujiandaa.
Aidha, hadi sasa hakuna taarifa rasmi za mabadiliko ya tarehe na si Morocco wala Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) wametoa taarifa rasmi kuhusu uamuzi huo.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Afrika Kusini,uamuzi huo umewashangaza waangalizi wengi hususani nchini Morocco ambapo tayari walikuwa wameandaa viwanja huko Rabat,Casablanca na Fez.
