DODOMA-Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimeibuka mshindi wa jumla katika shindano la Cyber Champions 2025/26, lililoratibiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), baada ya kutoa washindi wote wanne wa kitaifa katika mashindano hayo yaliyohusisha wanafunzi kutoka vyuo 29 nchini.
Washindi hao kutoka UDOM ni Boniface Ibrahimu, Martin George, Erick Sanga na Helidorice Macksenzius Mwalongo, ambao waliongoza kwa umahiri katika changamoto za kiusalama wa mtandao na kuipa UDOM heshima kubwa kitaifa.
Shindano la Cyber Champions lilianzishwa kwa lengo la kuibua vipaji, kutoa elimu ya vitendo, na kujenga kizazi kijacho cha wataalamu wa usalama wa mtandao kutoka vyuo vya elimu ya juu nchini.
Kwa mwaka huu, mashindano hayo yaliwakutanisha washiriki 1,226 waliosajiliwa kutoka vyuo takribani 29, ambapo baada ya hatua za awali na nusu fainali, washiriki 50 bora walifanikiwa kufika hatua ya fainali.
Kupitia changamoto halisi za kidijitali walizokabidhiwa, washiriki walipata fursa ya kuonesha uwezo wa vitendo, ubunifu, kazi ya timu na ujuzi wa kitaalamu, huku mashindano haya yakizidi kuimarisha nafasi yake kama jukwaa muhimu la kuandaa wataalamu wa usalama wa mtandao watakaolinda mustakabali wa mazingira ya kidijitali nchini Tanzania.
