KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Februari 11, 2026 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi nakufanya maamuzi yafuatayo;
Mechi Namba 082: Dodoma Jiji FC 1-0 Tanzania Prisons FC
Klabu ya Dodoma Jiji ya mkoani Dodoma imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la wachezaji wake kuchelewa kutoka kwenye chumba cha kuvalia kwa ajili ya kwenda kuanza mchezo kama ambavyo ratiba ya matukio ya mchezo imeelekeza.
Wachezaji hao walitoka chumbani saa 12:59 jioni badala ya saa 12:51 jioni jambo ambalo liliathiri mtiririko mzima wa matukio kuelekea kuanza kwa mchezo tajwa hapo juu kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:33 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Klabu ya Dodoma Jiji imepewa Onyo Kali kwa kosa la watoto waokota mipira kucheleweshakwa makusudi kurejesha mipira kiwanjani, matukio yaliyotafsiriwa kama hila ya kupoteza muda katika mchezo huo kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:7 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo. Klabu ya Dodoma Jiji imepewa Onyo Kali kwa kosa la gari la matangazo kuingia uwanjani wakati timu zikiendelea na mazoezi ya kupasha moto misuli kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:49 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo. Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi Namba 048: Azam FC 2-0 TRA United FC
Klabu ya Azam ya mkoani Dar es Salaam imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la wachezaji na baadhi ya viongozi wa benchi la ufundi kuonekana wakifanya kitendo kinachoashiria imani za kishirikina kuelekea mchezo tajwa hapo juu kwenye uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam. Wachezaji hao na viongozi walijikusanya kwenye lango la kuingia uwanjani (mita chache kutoka vyumba vya kuvalia) na kumwaga kimiminika, kitendo ambacho kililalamikiwa pia na timu pinzani (TRA United).
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Klabu ya Mashujaa ya mkoani Kigoma imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la wachezaji na maofisa wake wa ufundi kukataa kutumia chumba cha kuvalia baada ya kumalizika kwa kipindi cha kwanza cha mchezo tajwa hapo juu kwenye uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam, kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:20 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Mechi Namba 100: Coastal Union FC 1-1 TRA United FC
Klabu ya TRA United ya mkoani Tabora imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la wawakilishi wake kuchelewa kuwasili kwenye kikao cha kitaalam cha maandalizi ya mchezo (MCM) kwa dakika tano (5) pia kikosi hicho kilichelewa kuwasili uwanjani kwa dakika 10 kuelekea mchezo tajwa hapo juu kwenye uwanja wa Mkwakwani Tanga, kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:2(2.2) na 17:15 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo. Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Mechi Namba 101: Namungo FC 1-0 KMC FC
Klabu za Namungo (Lindi) na KMC (Dar es salaam) zimetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kila moja kwa kosa la kuchelewa kuwasili uwanjani kuelekea mchezo tajwa hapo juu kwenye uwanja wa Majaliwa uliopo Ruangwa mkoani Lindi, kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:15 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
KMC waliwasili uwanjani saa 11:43 jioni huku Namungo wakiwasili saa 11:44 jioni badala ya saa 11:30 jioni. Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Mechi Namba 105: Mtibwa Sugar FC 0-1 Tanzania Prisons FC
Klabu za Mtibwa Sugar (Morogoro) na Tanzania Prisons (Mbeya) zimetozwa faini ya Sh.5,000,000 (milioni tano) kila moja kwa kosa la wachezaji wake kuchelewa kutoka kiwanjani baada ya kumalizika kwa muda wa kufanya mazoezi ya kupasha moto misuli, kuelekea mchezo tajwa hapo juu kwenye uwanja wa Jamhuri uliopo mkoani Dodoma.
Jambo hilo ambalo ni kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:15 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za mchezo, lilisababisha mchezo huo kuchelewa kuanza. Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Mechi Namba 108: KMC FC 1-0 Mashujaa FC
Klabu ya KMC imepewa Onyo Kali kwa kosa la watoto waokota mipira kuchelewesha kwa makusudi kurejesha mipira kiwanjani, matukio yaliyotafsiriwa kama hila ya kupoteza muda katika mchezo huo kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:7 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi Namba 113: Pamba Jiji FC 3-0 Coastal Union FC
Klabu za Pamba Jiji (Mwanza) na Coastal Union (Tanga) zimetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kila moja kwa kosa la wachezaji wake kujichelewesha kwa makusudi kutoka kwenye vyumba vya kuvalia, kuelekea mchezo tajwa hapo juu kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Tukio hilo ambalo ni kosa kwa mujibu wa kanuni ya 17:33 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za mchezo, lilisababisha mchezo huo kuchelewa kuanza kwa dakika sita (6). Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Mechi Namba 114: Tanzania Prisons FC 0-0 Mashujaa FC
Klabu ya Tanzania Prisons ya mkoani Mbeya imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la kushindwa kuandaa kikamilifu mchezo tajwa hapo juu ambapo meneja wa uwanja huo aliwasili uwanjani dakika 12 kabla ya muda wa kuanza mchezo huku huduma muhimu kama umeme ikikosekana uwanjani hapo na mipira ya mechi ikiwa imefungiwa kwenye moja ya ofisi zilizopo uwanjani hapo hadi alipowasili.
Kutokuwepo kwa meneja wa uwanja wala viongozi wa Prisons kwa wakati uwanjani hapokulisababisha changamoto kadhaa wakati wa uwekaji alama za uwanjani baada ya mvua kubwa kunyesha.
Kosa hili limeainishwa kwenye kanuni ya 17:48 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo na adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi Namba 110: Mbeya Kwanza 3-2 Polisi Tanzania FC
Wachezaji wanne (4) wa klabu ya Polisi Tanzania, Christopher John Nyakanda, Alphonce Samweli Amos, Ibrahim Isihaka Ibrahim na Elisha Jissy Mwaihojo wamefungiwa michezo mitatu (3) na kutozwa faini ya sh. 1,000,000 (milioni moja) kila mmoja kwa kosa la kumpiga mwamuzi wa mchezo tajwa hapo juu kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:5(5.3) ya Championship kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.
Katika hatua nyingine, Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imemfutia adhabu ya kadi nyekundu mchezaji Baraka Michael Mwambule wa Polisi Tanzania baada ya kuthibitisha kuwa hakumpiga mwamuzi wala kushiriki katika vurugu hizo.Uamuzi huo ni kwa mujibu wa kanuni ya 12:7 ya Championship kuhusu Usimamizi wa Ligi.
Pia Afisa Usalama wa klabu ya Polisi Tanzania amefungiwa kwa kipindi cha miezi sita (6) na kutozwa faini ya Sh. 2,000,000 (milioni mbili) kwa kosa kumpiga mwamuzi wa mchezo tajwa hapo juu.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 46:3 ya Championship kuhusu Ushibiti kwa Viongozi.
Mechi Namba 125: Hausung FC 2-1 African Sports
Kocha msaidizi wa African Sports, Octavian Dismas amefungiwa michezo mitatu (3) na kutozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kumtukana na kumtolea lugha chafu mwamuzi wa akiba wa mchezo tajwa hapo juu.
Kocha huyo aliadhibiwa kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja na mwamuzi wa kati wa mchezo huo.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 45:2(2.1) ya Championship kuhusu Udhibiti kwa Makocha na Maofisa Wengine wa Ufundi.
Mechi Namba 133: Stand United FC 0-2 KenGold FC
Klabu ya Stand United ya mkoani Shinyanga imetozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la mashabiki wake kuingia kiwanjani (pitch) mara baada ya kumalizika kwa mchezo tajwa hapo juu kwenye uwanja wa Kambarage, Shinyanga, kinyume na matakwa ya kanuni na miongozo ya usalama viwanjani. Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:1 ya Championship kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Afisa Usalama wa klabu ya Stand United, Salum Juma na mkuu wa msafara wa klabu hiyo, Issa Shilla wamefungiwa kwa kipindi cha miezi sita (6) na kutozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kila mmoja kwa kosa la kuwashambulia kwa matusi na kujaribu kuwapigawaamuzi wa mchezo tajwa wakiwa wanaondoka uwanjani hapo baada ya mchezo kumalizika.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 46:3 ya Championship kuhusu Udhibiti kwa Viongozi.
Mechi Namba 136: B19 FC 4-1 African Sports
Klabu ya African Sports ya mkoani Tanga imetozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kushindwa kuwasilisha orodha ya viongozi wa benchi la ufundi waliopangwa kutumika katika mchezo tajwa hapo juu.
Kosa hili limeainishwa kwenye kanuni ya 17:6 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezona adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi Namba 18A: Dar City FC 1-2 Moro Kids
Klabu ya Dar City ya mkoani Dar es Salaam imetozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kikosi chake kuchelewa kufika kwenye uwanja wa TFF Center, Kigamboni kuelekea mchezo tajwa hapo juu.
Dar City iliwasili uwanjani hapo saa 8:50 mchana badala ya saa 8:30 mchana kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni ya 17:15 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo. Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi Namba 19B: IAA SC 3-1 Endument FC
Mchezaji Bryson Emanuel Urio wa klabu ya IAA ya Arusha amefungiwa kwa kipindi cha mwaka mmoja (1) na kutozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kubadili jina ili kufanikisha usajili wake kwenye klabu ya IAA.
Mchezaji alibainika kuwa anatumia jina laJoseph Ombeni katika usajili huo jambo ambalo si sahihi.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:9 ya First League kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.
Kocha John Zongwe wa klabu ya IAA ya Arusha amefungiwa kwa kipindi cha mwaka mmoja (1) na kutozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kumchezesha mchezaji Bryson Emanuel Urio ambaye ni batili kiusajili akitumia jina la Joseph Ombeni.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 45:2(2.10) ya First League kuhusu Udhibiti kwa Makocha na Maofisa Wengine wa Ufundi.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya IAA ya Arusha, Nadhiru Salumu Abdulnuru amepelekwa kwenye Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ili kujibu tuhuma za kutoa taarifa na nyaraka za uongo ili kufanikisha usajili wa mchezaji Bryson Emanuel Urio kwa jina la Joseph Ombeni.
Uamuzi huu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 46:13 ya First League kuhusu Udhibiti kwa Viongozi.
Klabu ya IAA imetozwa faini ya Sh. 1,200,000 (milioni moja na laki mbili) kwa kosa lakumtumia mchezaji Bryson Emanuel Urio kwa jina batili la Joseph Ombeni katika michezominne (4), ikiwa ni faini ya Sh. 300,000 kwa kila mchezo. Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:22 ya First League kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Mechi Namba 20A: Nyumbu FC 1-0 Pan African
Mtunza vifaa wa klabu ya Pan African, Saleh Nyembo ametozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kuendelea kusalia kiwanjani wakati wa mapumziko na kukataa kuingia
kwenye vyumba vya kuvalia kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:20 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi Namba 20B: Mapinduzi FC 2-1 Biashara United
Klabu ya Biashara United ya mkoani mara imetozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la maofisa wake kushindwa kuhudhuria kikao cha kitaalam cha maandalizi ya mchezo (MCM) kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:2(2.2) ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo. Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi Namba 22B: COPCO FC 1-3 Rhino Rangers
Mchezaji Bahati Posso wa klabu ya COPCO amefungiwa michezo mitatu (3) na kutozwa faini ya Sh. 300,000 (laki tatu) kwa kosa la kumshambulia kwa lugha ya matusi mwamuzi wa mchezo tajwa hapo juu kabla ya kuadhibiwa kwa kadi nyekundu, ambapo aliendelea kutoa matusi hata baada ya adhabu hiyo. Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:5(5.3) ya First League kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.
Daktari Isack Katambi wa klabu ya COPCO amefungiwa michezo mitatu (3) na kutozwa faini ya Sh. 300,000 (laki tatu) kwa kosa la kumshambulia kwa lugha ya matusi mratibu wa mchezo tajwa hapo juu, akipinga adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa mchezaji Bahati Posso.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 45:2(2.1) ya First League kuhusu Udhibiti kwa Makocha na Maofisa Wengine wa Ufundi.
Mechi Namba 24B: Endument FC vs Biashara United FC
Klabu ya Biashara United ya mkoani Mara imepoteza mchezo tajwa hapo juu na timu ya Endument FC ya Kilimanjaro imepewa ushindi wa mabao matatu (3) na alama tatu (3) kwa kosa la Biashara United kushindwa kufika kwenye uwanja wa BRM Complex uliopo mjini Moshi bila ya sababu za msingi na zinazokubalika hivyo kusababisha mchezo huo kushindwa kufanyika.
Sambamba na adhabu hiyo, Biashara United imetozwa faini ya Sh. 2,000,000 (milioni mbili), kutakiwa kulipa fidia ya maandalizi ya mchezo huo pamoja na kupokwa alama tatu (3) katika msimamo wa First League.
Pia Rais wa klabu ya Biashara United, Richardson Sakala amefungiwa kwa kipindi cha mwaka mmoja (1) kwa kosa la klabu yake kushindwa kufika uwanjani. Adhabu hizi ni kwa mujibu wa Kanuni ya 31:1(1.1, 1.2, 1.3 & 1.4) ya First League kuhusuKutofika Uwanjani.
Klabu ya Endument ya mkoani Kilimanjaro imetozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la wachezaji wake na viongozi wa benchi la ufundi kuonekana wakifanya vitendo vinavyoashiria imani za kishirikina kuelekea mchezo tajwa hapo juu kwenye uwanja wa Nyamagana, Mwanza.
Wachezaji hao na viongozi walionekana wakizunguka uwanja huku wakimwaga vimiminika, kuchukua mchanga ardhini na kuchimba na kufukia vitu visivyojulikana kwenye kona za uwanja huo.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:1 ya First League kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Mechi Namba 27B: Biashara United FC 1-1 IAA SC
Daktari wa klabu ya Biashara United, Abdallah Songe ametozwa faini ya Sh. 300,000 (laki tatu) kwa kosa la kumshambulia kwa maneno makali mwamuzi msaidizi wa mchezo tajwa hapo juu kabla ya kuadhibiwa kwa kadi nyekundu.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 45:2(2.5) ya First League kuhusu Udhibiti kwa Makocha na Maofisa Wengine wa Ufundi.






