ZANZIBAR-Benki Kuu ya Tanzania imeandaa mkutano wa Bodi ya Uthabiti wa Sekta ya Fedha (Financial Stability Board-FSB) uliofanyika katika Hoteli ya the Mora, Zanzibar tarehe 20 Februari 2026 ukiwahusisha Magavana, Manaibu Gavana na maofisa waandaamizi kutoka Benki Kuu za kusini mwa Jangwa la Sahara.

FSB ni chombo cha kimataifa ambacho hufuatilia na kutoa mapendekezo kuhusu mfumo wa fedha duniani kwa lengo la kuimarisha uthabiti wa Sekta ya Fedha kwa kuandaa miongozo ya kuzisaidia nchi wanachama kuboresha sekta hiyo.
Akizungumza wakati anafungua mkutano huo, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, alisema mkutano wa FSB unatoa fursa kwa benki kuu wanachama kujadili namna ya kudhibiti athari mbalimbali zinazoweza kusababisha sekta ya fedha ikafanya vibaya.
"Miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa katika mkutano huu ni pamoja na tathmini ya mwenendo wa viashiria vya uthabiti wa sekta kidunia na kikanda, athari za uthabiti wa sekta ya fedha unaotokana na na uhimilivu wa madeni, masuala ya Kifedha yasiyo ya Kibenki (NBFI) na Matumizi ya Teknolojia ya Akili Unde katika kuboresha utendaji wa sekta ya fedha pmoja na athari zake,"alisema Gavana Tutuba.
Aidha, alisisitiza kuwa ushiriki wa BoT katika mkutano huu unadhihirisha kuwa Benki Kuu inasimamia sekta ya fedha kwa mifumo inayokubalika kimataifa.
"Kupitia mkutano huu wananchi wanatakiwa kufahamu kuwa sisi BoT tunaendelea kusimamia sekta ya fedha kwa misingi na mifumo inayokubalika kimataifa na kwamba popote wanapohifadhi fedha zao watambue zipo salama na zinaendelea kutunzwa katika mifumo inayoendana na sheria na taratibu za kimataifa,"alieleza.
Miongoni mwa mafanikio ambayo BoT imeyapata kwa kuwa mwananchama wa FSB ni pamoja na kuanzishwa kwa muundo wa kutambua idadi ya benki muhimu, njia za kutathmini mwingiliano wa mifumo ya kifedha, tathmini ya majanga yatokanayo na mabadiko ya tabia ya nchi, muundo wa unyumbulifu wa kukabiliana na dharura, miongozo ya kujiandaa na majanga ya kifedha, miundo ya kusimamia sarafu mtandao,na vihatarishi vya taasisi za kifedha zisizokuwa za kibenki.






