NA DIRAMAKINI
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeshiriki katika Soko la Jumla la Fedha za Kigeni (IFEM) kwa mujibu wa Sera yake ya ushiriki katika soko la fedha za kigeni ya mwaka 2023, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza ukwasi katika soko hilo.
Katika ushiriki huo, Benki Kuu imeuza Dola za Marekani milioni 15.00 kupitia mnada wa ushindani, kwa kiwango cha wastani cha kubadilisha fedha cha Shilingi 2,587.85 kwa Dola moja ya Marekani.
Lengo la mnada huo lilikuwa ni kuimarisha upatikanaji wa fedha za kigeni na kuongeza utulivu katika soko.
Aidha,kwa mujibu wa matokeo ya mnada huo, kiasi kilichotangazwa kilikuwa Dola za Marekani milioni 15.00, huku kiasi kilichowasilishwa na washiriki kufikia Dola milioni 21.50, sawa na ziada ya maombi ya Dola milioni 6.50.
Hata hivyo, kiasi kilichokubaliwa kiliishia katika Dola milioni 15.00 kama ilivyopangwa.
Kiwango cha juu cha ushindani kilifikia Shilingi 2,596.57 kwa Dola moja ya Marekani, wakati kiwango cha chini cha ushindani kilikuwa Shilingi 2,552.06.
Vilevile kwa upande wa viwango vilivyokubaliwa, kiwango cha juu kilikuwa Shilingi 2,596.57 na kiwango cha chini Shilingi 2,582.00 kwa Dola moja ya Marekani. Pia,jumla ya benki 25 zilishiriki katika mnada huo, ambapo benki 18 zilifanikiwa kushinda.
.jpeg)
