NA DIRAMAKINI
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeshiriki katika Soko la Jumla la Fedha za Kigeni (IFEM) kwa mujibu wa Sera yake ya ushiriki katika soko la Fedha za Kigeni ya mwaka 2023, na kuuza Dola za Marekani milioni 14.75 kupitia mnada wa ushindani.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa leo Februari 12,2026 na Kurugenzi ya Masoko ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mauzo hayo yamefanyika kwa kiwango cha wastani cha kubadilisha fedha cha Shilingi 2,582.08 kwa Dola moja ya Marekani. Lengo la mnada huo lilikuwa kuongeza ukwasi katika soko la fedha za kigeni.
Aidha, katika mnada huo, kiasi kilichotangazwa kilikuwa Dola za Marekani milioni 15.00, huku kiasi kilichowasilishwa kikifikia Dola milioni 25.25. Hata hivyo, kiasi kilichokubaliwa kilikuwa Dola milioni 14.75.
Pia, kiwango cha juu cha ushindani kilikuwa Shilingi 2,592.50 kwa Dola moja ya Marekani na kiwango cha chini kilikuwa Shilingi 2,570.00. Kiwango cha juu kilichokubaliwa kilikuwa Shilingi 2,592.50, huku kiwango cha chini kilichokubaliwa kikiwa Shilingi 2,580.00.
Aidha,jumla ya benki 28 zilishiriki katika mnada huo, ambapo benki 18 zilifanikiwa kushinda.

