NA GODFREY NNKO
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Albert Chalamila amezindua Kamati ya Ushauri wa Kisheria ya Mkoa na Wilaya na Kliniki ya Sheria bila malipo Mkoa wa Dar es Salaam chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.


Uzinduzi huo umefanyika leo Februari 16,2026 na utadumu hadi Februari 22,2026 katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam ambapo wataalamu wa sheria watatoa usaidizi wa kisheria kwa wiki moja kwa wananchi.
RC Chalamila ameipongeza, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuratibu zoezi hili muhimu ambalo anasema lina manufaa makubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Amesema, kutokana na watu wengi kukosa uelewa wa kisheria, katika mazingira ya uraiani pamekuwepo malumbano mengi ambayo huwa yanakosa muafaka, lakini kupitia kliniki hizi na elimu ya kisheria itasaidia wengi kuwa na ufahamu wa kutosha.
Kwa kukosa uelewa wa kisheria, RC Chalamila amesema kuwa,"...ni ukweli kwamba watu wengi katika masuala ya kisheria huwa wanagombana sana, hivyo ni mimpongeze Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuja na programu hii ambayo itasaidia watu wengi ambao hawana uelewa wa kisheria huko mitaani."
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Naye Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Samwel Maneno amesema kuwa, zoezi hilo linaendeshwa na ofisi yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ili wananchi wanaokutana na changamoto za kisheria kila siku ziweze kupatiwa ufumbuzi bure.
Amesema, ofisi hiyo ina jukumu la kuwasimamia mawakili wa Serikali katika ofisi zote za umma ili kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa manufaa ya umma na Taifa kwa ujumla.
Pia, wanajukumu la kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi ili waweze kupata uelewa wa kutosha na namna bora ya kuwasaidia kupata ufumbuzi wa changamoto zao.
Lengo la kliniki hizi ni kusogeza huduma za kisheria karibu zaidi na wananchi ili waweze kupata ushauri na msaada wa kisheria kwa urahisi.
Pia,kamati zimeanzishwa ili kutoa ushauri kwa wananchi, watumishi na viongozi wa umma katika kutatua changamoto za kisheria ngazi ya mikoa na wilaya.
Miongoni mwa manufaa ya kamati hizi ni kupunguza migogoro dhidi ya serikali, malalamiko ya kisheria, vitendo vinavyokiuka sheria na taratibu, pamoja na kutoa elimu ya sheria kwa umma.
Amesema kwa sasa, kamati hizi zimeshazinduliwa katika mikoa ya Dodoma, Kilimanjaro, Singida, Manyara na Simiyu ambapo wananchi zaidi ya 5,000 wamepata usaidizi wa kisheria huku migogoro ya ardhi ikiongoza.
TLS
Mwakilishi wa Sheria ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), amesema kuwa, moja ya jukumu lao ni kusaidia umma chini ya Kifungu Na.4 cha Sheria ya TLS, hivyo wataendelea kushirikiana na Serikali ili kuendelea kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi nchini.
Pia, amepongeza uzinduzi wa kamati hiyo huku akiomba zoezi hilo kuwa endelevu ili kuweza kuwahudumia wananchi na makundi mbalimbali nchini.
TPBA
Kwa upande wake,Makamu wa Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali (TPBA),Wakili Debora Mcharo amesema, chama hicho kinatambua umuhimu wa uzinduzi wa zoezi hili ambalo limeandaliwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali huku wakiahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha wananchi wanapata msaada wa kisheria na ushauri bila malipo.
Amesema, chama hicho kinaendelea kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye pia ni mlezi wa chama chao ili kuhakikisha wanaleta matokeo chanya kwa kuhakikisha wananchi wanapata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za kisheria.
Wabunge
Naye Mbunge wa Ukonga, Mheshimiwa Bakari Shingo ambaye amewawakilisha wabunge wa Dar es Salaam amesema,kliniki hii ni muhimu zaidi kwani itasaidia wananchi kupata ufumbuzi wa changamoto za kisheria zinazowakabili katika nyanja mbalimbali.
Aidha, kwa niaba ya wabunge wenzake wameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa kikamilifu katika kuwahudumia wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Mheshimiwa Shingo ametoa mfano kuwa, moja ya changamoto kubwa ya kisheria inayowakabili wananchi wa mkoa na jimbo lake kwa ujumla ni migogoro ya ardhi ambalo anaamini kuwa, kupitia wanasheria wabobezi wananchi watapata msaada wa kisheria bure.