Dkt.Donatus Boniphace Tsete afunguliwa mashauri matatu kwa makosa saba ikiwemo Uhujumu Uchumi

KILIMANJARO-Dkt.Donatus Boniphace Tsete ambaye ni mratibu wa kifua kikuu na ukoma Hospitali ya Taifa ya Kibong'oto iliyopo Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro amefunguliwa mashauri matatu kwa makosa saba ikiwemo Uhujumu Uchumi.
‎Mashauri hayo namba 2831, 2834 na 2837 ya mwaka 2026 yamefunguliwa Februari 10,2026 na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Wilaya ya Siha mbele ya
Hakimu Mkazi mfawidhi wa Mahamaka ya Wilaya ya Siha, Mhe.Jasmin Abduli.

Mashauri hayo ni kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dhidi ya mshtakiwa Dkt.Donatus Boniphace Tsete.

‎Dkt.Tsete anakabiliwa na makosa saba kwenye kila shauri ambapo katika kosa la kwanza anashtakiwa kwa matumizi Mabaya ya Mamlaka kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11/ 2007 ikisomwa pamoja na Aya ya 21, Jedwali la Kwanza, kifungu 57(1) na Kifungu cha 60(2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa Sura ya 200 marejeo ya Mwaka 2019.

Inadaiwa kuwa,kwa kutumia cheo chake alifuja fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya usugu wa dawa za kifua kikuu (Drug- resistant Tubercolosis Mentorship) kwa Halmashauri ya Wilaya ya Same shilingi 5,082,000, Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro shilingi 5,061,000 na shilingi 5,490,000 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha kwenye kesi tatu.

‎Kosa la Pili likiwa ni Kughushi Kinyume na kifungu cha 333, 335(1) na 337 cha Kanuni za Adhabu sura ya 16 marejeo ya Mwaka 2022.

Aligushi saini kwenye attendance kuonesha kwamba washiriki wa mafunzo walisaini kulipwa fedha hizo.

‎Aidha,kosa la tatu likiwa ni kuandaa nyaraka zenye maelezo ya uongo kinyume na kifungu cha 342 na 337 cha Kanuni za Adhabu sura ya 16 marejeo ya Mwaka 2022.

Nyaraka zenye maelezo ya uongo ni hati ya malipo na viambatisho vyake ambavyo ni dokezo sabili na pay list.

Kosa la nne ni kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri kinyume na kifungu cha 22 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa sura ya 329 R.E 2019 hati ya malipo na viambatisho vyake ambavyo ni dokezo sabili, pay list.

Kosa la tano ni ubadhirifu wa fedha jumla ya shilingi 15,633,000 kinyume na kifungu cha 28 (1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

Kosa la sita kuisababishia mamlaka hasara ya shilingi 15,633,000 kinyume na Aya ya 21 ya jedwali la kwanza kifungu cha 57 (1) na 60 (2) vya sheria ya uhujumu uchumi sura ya 200 toleo la 2019.

Kosa la saba ni kuwasilisha nyaraka zenye maelezo ya uongo kinyume na kifungu cha 342, na 337 vya sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 toleo la mwaka 2019.

Mshtakiwa amekana mashtaka yote na amekidhi vigezo vya dhamana vilivyowekwa na Mahakama, hivyo yupo nje kwa dhamana na kesi yake imeahirishwa hadi Februari 23, 2026.

Katika hatua nyingine mshtakiwa ameiomba Mahakakama afanye 'plea bargaining' kwenye mashauri yote matatu, aliambiwa aandike barua kwa Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Kilimanjaro kuhusu ombi hili, ameshaandika barua hiyo anasubiri majibu.

Kesi hizo tatu zinaendeshwa na mawakili wa Serikali Bi. Suzan Kimaro na Bw. Bernard Ndamallya kutoka TAKUKURU.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here