NA LWAGA MWAMBANDE
NDOA ni taasisi muhimu katika maisha ya mwanadamu na msingi wa ustawi wa jamii. Kwa mujibu wa mafundisho ya dini kama Ukristo na Uislamu, ndoa ni agano takatifu linalojengwa juu ya heshima, uwajibikaji na upendo.
Hivyo, ni muhimu kwa kijana wa kiume kutafuta mchumba na kuoa kwa kuzingatia maadili mema.Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, ndoa humjenga kijana kuwa mtu mwenye nidhamu na uwajibikaji.
Pia,humwezesha kuwa kiongozi wa familia na kushiriki kikamilifu katika malezi bora ya watoto. Pili, hulinda heshima na afya yake kwa kumuepusha na mienendo isiyofaa kijamii na kiafya.
Kwa hiyo, kijana anapaswa kuoa si kwa shinikizo la jamii, bali kwa utayari wa kiakili, kiuchumi na kimaadili. Ndoa yenye maadili hujenga familia imara na jamii yenye ustawi.Endelea;
1. Ee kijana wa kiume, wewe ulopendelewa,
Kutafuta ujitume, mke aweze twaliwa,
Ni vipi wewe ugome, hata pozi kuishiwa,
Mabinti ni wengiwengi, mbona hujichagulii?
2. Kutongoza kazi yako, mbona wewe wachelewa,
Unakaa ukouko, majira wayaelewa,
Hujui wako ujiko, wako mwenyewe chaguwa,
Mabinti ni wengiwengi, mbona hujichagulii?
3. Umri unaridhisha, naye Mungu umepewa,
Tena unayo maisha, unakula unatawa,
Nini chakuchelewesha, familia kuwa sawa,
Mabinti ni wengiwengi, mbona hujichagulii?
4. Kipato umejaliwa, unakwenda sawasawa,
Wajuwa wasubiriwa, binti umuweke sawa,
Mbona sasa wachelewa, ili apate fikiwa,
Mabinti ni wengiwengi, mbona hujichagulii?
5. Mungu amekuamini, ni wewe unangonjewa,
Umtafute mwandani, yule unayenogewa,
Yuko na wewe jirani, asubiri kuambiwa,
Mabinti ni wengiwengi, mbona hujichagulii?
6. Ni furaha kwa wazazi, uchumba wakismbiwa,
Hapo inabaki kazi, nyie kuzidi ombewa,
Mwanaume weka wazi, nani kwako muolewa,
Mabinti ni wengiwengi, mbona hujichagulii?
6. Binti mnaongojea, na waume kutokewa,
Na maombi endekea, Mungu anawaelewa,
Mchumba akitokea, mara mtamuelewa,
Mabinti ni wengiwengi, mbona hujichagulii?
7. Waharibifu washenzi, muweze kuwaelewa,
Hao wala si wapenzi, msijekuchafuliwa,
Tena mtambue wazi, na sisi mnaombewa,
Mabinti ni wengiwengi, mbona hujichagulii?
8. Mungu wetu twakuomba, uinue uelewa,
Vijana wanaotamba, waoe na kuolewa,
Ili wazidi kuumba, wajibu tuliopewa,
Mabinti ni wengiwengi, mbona hujichagulii?
(1 Wakorintho 7:9b)
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602