ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewataka Waislamu na wananchi wote kuutumia Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuimarisha uchamungu, mshikamano wa kijamii na kudumisha amani na utulivu nchini.
Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza kuendelezwa kwa mafunzo ya dini, kusaidiana na kutoa sadaka kwa wahitaji, pamoja na kuhimiza wafanyabiashara kutopandisha bei za bidhaa muhimu katika kipindi hiki.
Aidha, ameeleza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa muhimu na kuvitaka vyombo husika kusimamia mwenendo wa bei na usafi wa mazingira wakati wa Ramadhani.
Rais Dkt. Mwinyi amewaomba wananchi kuendelea kuishi kwa amani, kuheshimiana na kuzingatia sheria, huku akimuomba Mwenyezi Mungu awajaalie Waislamu wote kutekeleza ibada ya saumu kwa ikhlasi.
