Kwa nini Watanzania wengi wanapendelea kujenga nyumba zenye mapaa marefu?

NA DIRAMAKINI

MIAKA ya karibuni hapa nchini Tanzania, kumekuwepo mwelekeo wa namna yake unaoonekana wazi katika sekta ya ujenzi hususani ongezeko la nyumba zenye mapaa marefu, hasa paa la mteremko mkali (hip or pyramid roof).
Picha na Mtandao.

Kutoka mijini hadi vijijini, muundo huu umeendelea kushika nafasi ya juu katika ramani za wasanifu majengo na chaguo la wamiliki wa nyumba.

Mwelekeo huu haujatokana na fasheni pekee, bali umejengwa juu ya misingi imara, ustahimilivu wa hali ya hewa, urembo na uzoefu wa kitaalamu wa mafundi wa ndani.

Moja ya sababu kuu zinazofanya paa la mteremko mkali kupendwa ni uwezo wake mkubwa wa kukabiliana na hali ya hewa ya Tanzania.

Nchi yetu hupata mvua kubwa katika baadhi ya maeneo, hasa kipindi cha masika. Paa la mteremko mkali huruhusu maji ya mvua kupita kwa haraka bila kutuama juu ya bati au vigae, jambo linalopunguza hatari ya kuvuja na kuongeza maisha ya paa.

Zaidi ya hilo, muundo wa hip roof hauna ukuta wa pembeni unaojulikana kama gable ambao mara nyingi hukamata upepo kwa nguvu.

Kutokana na umbo lake lenye pande zinazokutana juu kwa juu, upepo husambaa sawasawa badala ya kusukuma ukuta mmoja moja kwa moja.

Hivyo, nyumba zenye paa la aina hii huwa na ustahimilivu mkubwa dhidi ya upepo mkali, hasa katika maeneo ya pwani na nyanda za juu.

Sehemu ya paa inayotoka nje ya ukuta (overhang) ni kipengele kingine muhimu kinachochangia umaarufu wa mapaa marefu.

Overhang hulinda kuta dhidi ya mvua inayoanguka kwa mwelekeo wa upepo pamoja na jua kali.

Kwa kufanya hivyo, hupunguza uharibifu wa rangi ya nje, kupasuka kwa plasta, na hata kuingia kwa unyevunyevu ndani ya kuta.

Katika mazingira ya joto kali, kivuli kinachotolewa na overhang husaidia pia kupunguza joto linalopiga moja kwa moja kwenye kuta na madirisha.

Hii si tu kwamba huongeza maisha ya jengo, bali pia hupunguza gharama za matengenezo ya mara kwa mara.

Kwa upande wa urembo, paa la mteremko mkali lina symmetry inayovutia macho. Hata kama ukubwa wa eneo la nyumba (footprint) ni mdogo, muundo wa paa unaweza kuifanya ionekane ya hadhi ya juu na ya thamani kubwa.

Ndiyo maana katika ramani nyingi za kisasa za Tanzania, hasa za nyumba za familia moja (bungalow), hip roof hupewa kipaumbele.

Muonekano huu wa kifahari huongeza thamani ya soko ya nyumba. Kwa mnunuzi au mpangaji mtarajiwa, sura ya nje ya jengo huwa ni kigezo muhimu cha kwanza cha kuvutia.

Hivyo, paa refu na lenye umbo lililosawazika huchangia katika taswira chanya ya mali husika.

Kutokana na kuwa na pande (faces) nyingi, paa la aina hii hutoa fursa ya ubunifu katika matumizi ya mabati ya rangi au vigae vya kisasa.

Wamiliki wa nyumba wanaweza kuchagua rangi inayolingana na rangi ya kuta, au hata kuchanganya rangi na texture tofauti ili kuongeza mvuto wa jengo.

Katika soko la Tanzania, mabati ya rangi yamekuwa yakipatikana kwa wingi, jambo linalowapa wateja uhuru wa kuchagua mitindo inayowiana na machaguo yao.

Hivyo, paa refu si tu kinga dhidi ya mvua na jua, bali pia ni kipengele cha mapambo kinachobeba utambulisho wa nyumba.

Sababu nyingine isiyopuuzwa ni uzoefu wa mafundi wa ndani. Mafundi wengi wa Tanzania wamezoea zaidi kujenga paa la hip kuliko aina nyingine kama gable au flat roof.

Uzoefu huu huleta ufanisi katika utekelezaji, hupunguza makosa ya kiufundi, na kuongeza imani kwa mmiliki wa nyumba.

Kwa kuwa mbinu zake zimezoeleka, upatikanaji wa vifaa na uelewa wa miundo ya mbao au chuma kwa ajili ya trusses huwa rahisi zaidi. Hii huchangia pia katika kudhibiti gharama na muda wa ujenzi.

Muundo wa paa refu huruhusu uwekaji wa matundu ya hewa (vents) kwenye ridge au kwenye soffit.

Mfumo huu wa uingizaji hewa husaidia kupunguza mkusanyiko wa joto ndani ya dari, hasa katika maeneo yenye hali ya joto kali kama vile mikoa ya ukanda wa pwani na nyanda ya kati.

Kwa kuruhusu hewa,joto kupaa juu na kutoka nje, mazingira ya ndani ya nyumba hubaki na hali ya hewa inayovumilika zaidi. Hii inaweza kupunguza utegemezi wa viyoyozi au feni, na hivyo kupunguza matumizi ya umeme.

Kwa kuzingatia mambo ya kiusalama, kiuchumi, kimazingira na kimuonekano, si ajabu kuona Watanzania wengi wakichagua kujenga nyumba zenye mapaa marefu.

Ni muundo unaoendana na hali ya hewa ya nchi, unaoongeza thamani ya jengo, na unaotekelezeka kwa urahisi kutokana na uzoefu wa mafundi wa ndani.

Kadiri sekta ya ujenzi inavyoendelea kukua na ubunifu kuongezeka, inaonekana wazi kuwa paa la mteremko mkali litaendelea kuwa chaguo linalopendwa nasi tu kwa sababu ya mvuto wake wa nje, bali pia kwa faida zake za muda mrefu kwa mmiliki wa nyumba nchini Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here