Wizara ya Afya yatoa tahadhari dhidi ya Influenza,UVIKO-19,Dengue na Kipindupindu

NA DIRAMAKINI

WIZARA ya Afya imetoa tahadhari kwa umma kuhusu ongezeko la magonjwa ya mlipuko hususan mafua makali ya Influenza, UVIKO-19, Homa ya Dengue na Kipindupindu, na kusisitiza umuhimu wa wananchi kuzingatia kikamilifu hatua za kinga ili kudhibiti maambukizi.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Februari 25,2026 na Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt.Grace E. Magembe.

Kupitia taarifa hiyo, Dkt.Magembe amesema, wizara imeendelea kufuatilia mwenendo wa magonjwa ya mlipuko na kubaini kuwepo kwa ongezeko la wagonjwa wa mafua makali ya Influenza na UVIKO-19 katika kipindi hiki.

Ameeleza kuwa,magonjwa hayo huambukizwa kwa njia ya hewa kupitia matone madogo yanayotoka kwa mtu aliyeambukizwa anapokohoa, kupiga chafya au kuzungumza.

Aidha, maambukizi yanaweza kutokea kwa kugusa nyuso au mazingira yaliyochafuliwa na majimaji kutoka kwa mgonjwa. Dalili zake ni pamoja na homa kali, kikohozi, maumivu ya kichwa na mwili, mafua, uchovu na wakati mwingine kuishiwa pumzi.

Kwa mujibu wa takwimu za ufuatiliaji, kila mwaka kati ya mwezi Novemba na Aprili, kumekuwa na ongezeko la magonjwa hayo nchini na duniani kote.

Kutokana na hali hiyo, Wizara imezitaka jamii kuchukua tahadhari zifuatazo ikiwemo kufunika pua na mdomo wakati wa kukohoa au kupiga chafya.

Pia,kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono; kuepuka misongamano isiyo ya lazima; kuvaa barakoa unapokuwa na dalili au unapomhudumia mwenye dalili.

Sambamba na kuwahi katika vituo vya huduma za afya kwa ushauri na matibabu stahiki badala ya kujitibu au kutumia antibiotiki bila ushauri wa wataalamu.

Wizara pia imeonya juu ya hatari ya Homa ya Dengue, hasa katika kipindi cha mvua za masika ambapo mazalia ya mbu huongezeka.

Ugonjwa huo huenezwa na mbu aina ya Aedes anayezaliana kwenye maji yaliyotuama na hupenda kuuma nyakati za asubuhi, mchana na jioni.

Dalili zake ni homa kali, maumivu ya kichwa na viungo, maumivu nyuma ya macho pamoja na uchovu, hali inayoweza kufanana na malaria.

Wananchi wametakiwa kutokomeza mazalia ya mbu kwa kufukia madimbwi ya maji yaliyotuama, kuondoa makopo, matairi chakavu na vyombo vinavyoweza kuhifadhi maji yasiyotiririka.

Pia, wametakiwa kujikinga kwa kuvaa nguo ndefu, kutumia dawa za kufukuza mbu na kuweka nyavu kwenye madirisha na milango.

Kuhusu Kipindupindu, Wizara imebainisha kuwa nchi imekumbwa na mlipuko uliogusa takribani mikoa yote isipokuwa Kilimanjaro na Njombe, hata hivyo kwa takribani mwezi mmoja uliopita hakujaripotiwa mgonjwa mpya.

Pamoja na mafanikio hayo, bado kuna hatari kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na uwepo wa maambukizi katika nchi jirani.

Katika kuzuia Kipindupindu, wananchi wametakiwa kuchemsha au kutibu maji ya kunywa kwa dawa maalumu na kuyatunza katika vyombo safi.

Aidha,kunawa mikono kwa maji na sabuni kabla ya kula na baada ya kutoka chooni; kuosha matunda na vyakula kwa maji safi; kujenga na kutumia vyoo bora; kuepuka kuchafua vyanzo vya maji; na kutunza mazingira kwa ujumla.

Serikali imeeleza kuwa, itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa magonjwa hayo na kutoa taarifa mara kwa mara kulingana na mabadiliko ya hali ya maambukizi, huku ikiendelea kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa wagonjwa wote.

Wizara imewahimiza wananchi kushirikiana na mamlaka za afya kwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa, ili kulinda afya binafsi na ya jamii kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here