Kwaheri Koplo wa Polisi, CPL Tumsifu Wilson Kileo

MWANZA-Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda, Februari 16,2026 aliongoza mamia ya waombolezaji, wakiwemo Maafisa, Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali, katika kuuaga mwili wa Koplo wa Polisi (CPL) Tumsifu Wilson Kileo, aliyefariki dunia Februari 13, 2026 katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando alipokuwa akipatiwa matibabu.
Askari huyo alifariki dunia kutokana na kugongwa na daladala iliyoacha njia wakati akitekeleza majukumu yake ya kuongoza magari.

Akizungumza na waombolezaji Mhe. Mtanda aliwahimiza askari na waombolezaji kumuenzi marehemu kwa kuyaishi mema aliyoyaacha katika kulitumikia Jeshi la Polisi na jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafungwa, akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, alitoa pole kwa familia, ndugu na jamaa kwa msiba huo mzito huku akisema kuwa CPL Tumsifu alikuwa mtumishi mwenye weledi na mchapa kazi ambaye bado alihitajika katika nguvu kazi ya Jeshi la Polisi.

Aidha Kamanda Mutafungwa alisema ajali hiyo ilitokea Februari 10,2026 majira ya saa 2.00 asubuhi katika mzunguko wa Mwanza Hoteli.

Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Buhongwa, Lucas Baskely ambaye aliongoza ibada ya kumuombea CPL Tumsifu aliwaasa waendesha vyombo vya moto kutotumia vyombo hivyo kama silaha ya kuua watumiaji wengine wa barabara.
Mwili wa marehemu CPL Tumsifu unatarajiwa kuzikwa Februari 17, 2026 katika Kijiji cha Lyamungo mkoani Kilimanjaro.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here