NA GODFREY NNKO
SERIKALI imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta ya anga kwa kuimarisha miundombinu ya viwanja vya ndege ili kukidhi viwango vya kimataifa, sambamba na kukuza utalii na biashara kupitia uimarishaji wa usalama na utulivu nchini.
Kauli hiyo imetolewa Februari 26, 2026 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.Bw.Msigwa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo alikuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Serikali katika siku 100 za uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akibainisha mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya usafiri wa anga.
Katika kuimarisha sekta hiyo, amesema Wizara ya Uchukuzi kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imefanikiwa kuvutia mashirika saba mapya ya ndege ya kimataifa kuanzisha safari nchini.
Mashirika hayo ni Airlink,Zambia Airways, Saudia,Air France,Skyward Express,South African Airways na Xerin Air.
Msigwa amesema, hatua hiyo imeongeza ushindani wa kibiashara, kurahisisha safari za kimataifa na kuchochea ukuaji wa utalii pamoja na biashara, huku ikiimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha usafiri wa anga katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Aidha, kutokana na maboresho ya miundombinu na mifumo ya usalama, Msigwa amesema Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere pamoja na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, vimetambuliwa kimataifa kwa tuzo za ubora na usalama.
Mafanikio hayo yanaendelea kuimarisha hadhi ya Tanzania katika sekta ya anga duniani.
Akizungumzia kuhusu takwimu za safari za ndege,abiria na mizigo, Msemaji Mkuu wa Serikali amesema kuwa, TAA imeendelea kukusanya na kuchambua takwimu rasmi za uendeshaji wa viwanja vya ndege 61 inavyovisimamia nchini.
Takwimu hizo zinahusu idadi ya safari za ndege, abiria na tani za mizigo,na hutumika kama kiashiria muhimu cha kupima uimara wa sekta ya usafiri wa anga pamoja na kusaidia maamuzi ya uwekezaji, ukarabati, upanuzi na uboreshaji wa miundombinu.
Akitoa ulinganisho wa mwaka wa fedha 2024/2025 na 2023/2024, Msigwa amesema, safari za ndege 2023/2024 zilikuwa 148,897 na mwaka 2024/2025 safari zilikuwa 149,835 ikiwa ni ongezeko la asilimia 0.6.
Kwa upande wa idadi ya abiria mwaka 2023/2024 amesema,abiria walikuwa milioni 5.15 huku 2024/2025 wakiwa abiria milioni 5.25 ambapo ongezeko ni asilimia 2.0.
Msigwa akizungumzia upande wa tani za mizigo mwaka 2023/2024 amesema zilikuwa 34,620 huku mwaka 2024/2025 zikiwa tani 37,683 sawa na ongezeko la asilimia 8.8.
Takwimu hizo zinaonesha kuwa,licha ya ongezeko dogo la safari za ndege, kumekuwepo ukuaji mkubwa zaidi katika idadi ya abiria na hasa mizigo, hali inayoashiria kuimarika kwa shughuli za kiuchumi na biashara zinazotegemea usafiri wa anga nchini.
Akizungumzia mwenendo wa mwezi Julai hadi Desemba,2025 ukilinganishwa na Julai hadi Desemba,2024 amesema,sekta imeendelea kuimarika.
Msigwa amesema, safari za ndege katika kipindi cha Julai hadi Desemba,2024 zilikuwa 83,647 huku Julai hadi Desemba,2025 zikiwa 91,760 sawa na ongezeko la asilimia 10.
Kwa upande wa abiria katika kipindi cha Julai hadi Desemba,2024 walikuwa 2,819,912 na Julai hadi Desemba 2025 walikuwa 3,071,081 sawa na ongezeko la asilimia tisa.
Mwenendo huo unaonesha mwelekeo chanya wa ukuaji unaochochewa na kuimarika kwa safari za ndani na kimataifa, pamoja na kuongezeka kwa mahitaji ya huduma za usafiri wa anga.
Kwa ujumla, takwimu hizo zinathibitisha kuimarika kwa sekta ya usafiri wa anga nchini na kutoa msingi imara wa mipango ya maendeleo ya baadaye ya viwanja vya ndege, huku zikionesha mchango wake katika kukuza uchumi wa Taifa.
Ikumbukwe kuwa, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/25 na nusu ya mwaka 2025/26, Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika uboreshaji na upanuzi wa miundombinu ya viwanja vya ndege nchini kwa lengo la kuongeza ufanisi, usalama na ubora wa huduma za anga.
Pia,Serikali imeendelea kuimarisha usalama katika maeneo ya viwanja vya ndege, kwa kununua mashine za kisasa 13 za ukaguzi wa abiria na mizigo na kuzifunga katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Uwanja wa Kigoma, Shinyanga, Tanga, Lake Manyara na Iringa.
Msemaji Mkuu wa Serikali amesema, hatua hizi zimeongeza ubora wa huduma na kuruhusu viwanja husika kutoa huduma mchana na usiku.
Tags
ATCL Tanzania
Gerson Msigwa
Habari
Kimataifa
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA)
Wizara ya Uchukuzi Tanzania



