Mtambo wa Oksijeni waokoa maisha ya wananchi Lushoto

TANGA-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe ameshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuokoa maisha yake na wananchi wa Lushoto kwa kutoa fedha zilizowezesha kupatikana kwa mtambo wa kuzalisha hewa tiba ya oksijeni katika Hospitali ya Wilaya ya Lushoto.
Prof. Shemdoe ametoa shukrani hizo leo kwa Mhe. Rais wakati alipopewa fursa na Mhe. Waziri Mkuu ya kuwasalimia wananchi wa Lushoto, mara baada ya Mhe. Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba kuzindua rasmi mtambo wa kuzalisha hewa tiba ya oksijeni katika Hospitali ya Wilaya ya Lushoto uliowekwa na Serikali ili kuboresha utoaji wa huduma za tiba kwa wananchi.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutuletea Shilingi Bilioni 5 zilizotuwezesha kupata vituo vya afya, zahanati pamoja na ununuzi wa mtambo huu wa kuzalisha hewa tiba ya oksijeni uliotuzindulia leo,” ameeleza Prof. Shemdoe.
Prof. Shemdoe amemueleza Mhe. Waziri Mkuu kuwa, anatambua na kuthamini umuhimu wa mtambo wa kuzalisha hewa tiba ya oksijeni kwani mwaka 2020 hewa ya Oksijeni iliokoa maisha yake alipolazwa Hospitali ya Benjamini Mkapa, na Septemba 11, 2025 alisafirishwa kwa ajili ya matibabu akiwa ametundikiwa oksijeni kutoka Hospitali ya Wilaya ya Lushoto kwenda Hospitali ya Muhimbili.

Mhandisi Vifaa Tiba wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Bw. Paschal Protace amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha kupatikana na mtambo unaozalisha hewa tiba ya oksijeni, ambayo inatumika kuwahudumia watoto njiti na akina mama wajawazito ambao wanauhitaji mkubwa wa hewa tiba hiyo ya oksijeni.
Kwa upande wake, mkazi wa Lushoto Bi. Khadija Rashidi ameshukuru Mungu kwa kujifungua salama na amemshukuru pia Mhe. Rais kwa kuwezesha uwepo wa vifaa tiba ambavyo ni mtambo wa kuzalisha hewa tiba ya oksijeni na kifaa cha kuhifadhia watoto njiti (incubator) vilivyomsaidia mtoto wake kuhifadhiwa ili kupata joto na hewa safi ya oksijeni mpaka alipoimarika kiafya.

Naye Muuguzi wa Hospitali ya Wilaya ya Lushoto Bi. Theodora Tesha amesema, watoto wengi walikuwa wakipoteza maisha kabla ya kuwekwa kwa mtambo wa kuzalisha hewa tiba ya oksijeni, lakini hivi sasa idadi ya vifo imepungua kwa kiasi kikubwa na ameongeza kuwa hawajawahi kupungukiwa oksijeni kwa ajili ya kuwahudumia watoto na akina mama wajawazito.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here