ARUSHA-Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA) imeibuka mshindi na kutunukiwa Tuzo ya Mamlaka Bora yenye Uimara wa Kifedha (Financial Stability) kwa mwaka 2025, ikiwa ni utambuzi wa mafanikio yake katika usimamizi madhubuti wa rasilimali na uendeshaji wenye tija.
Tuzo hiyo ilikabidhiwa rasmi Februari 23, 2026, katika hafla ya Usiku wa Tuzo za Wizara ya Maji iliyofanyika katika Hoteli ya Ngurudoto jijini Arusha.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Waziri wa Maji, Jumaa Hamidu Aweso, aliyekabidhi tuzo kwa niaba ya Wizara ya Maji.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi tuzo hiyo, Mheshimiwa Aweso alieleza kuwa,lengo la tuzo hizo ni kutambua na kuhamasisha utendaji bora wa mamlaka za maji, wasimamizi na watendaji walioonesha mafanikio makubwa katika sekta hiyo nchini.
Pia,alisisitiza kuwa, serikali itaendelea kuzipima na kuzitambua taasisi zinazotekeleza majukumu yake kwa weledi, uwajibikaji na ubunifu, ili kuongeza ufanisi wa huduma za maji safi na usafi wa mazingira kwa wananchi.
Kwa upande wake, MUWSA imeeleza kuwa, tuzo hiyo ni heshima kubwa kwa taasisi pamoja na wadau wake wote, na ni uthibitisho kuwa inaendelea kusimamia rasilimali zake kwa umakini, uwazi na ufanisi wa hali ya juu.
“Tuzo hii ni matokeo ya juhudi za pamoja za menejimenti, watumishi na wadau wetu. Inatupa ari mpya ya kuendelea kuboresha huduma na kuhakikisha tunadumisha nidhamu ya kifedha kwa manufaa ya wananchi wa Moshi na maeneo jirani,” ilieleza sehemu ya taarifa ya mamlaka hiyo.
MUWSA imewashukuru wadau wake kwa ushirikiano wao endelevu na kuahidi kuimarisha zaidi mifumo ya utoaji huduma, ukusanyaji wa mapato na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuzingatia misingi ya uwazi na uwajibikaji.
Aidha,kupatikana kwa tuzo hiyo kunaiweka MUWSA katika nafasi ya mfano wa kuigwa miongoni mwa mamlaka za maji nchini, hususan katika eneo la uthabiti wa kifedha na usimamizi wa rasilimali za umma.
