TABORA-Aliyekuwa Diwani wa Kata ya Itilo na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Nzega mkoani Tabora, Paschal Kigalu (56), amefariki dunia kufuatia ajali ya gari iliyotokea juzi wilayani humo.
Taarifa za kifo hicho zimethibitishwa wakati wa ibada ya mazishi iliyofanyika jana katika Kijiji cha Itilo, Kata ya Itilo, Wilayani Nzega, ambapo viongozi wa chama na serikali pamoja na wananchi walikusanyika kumlaki marehemu kwa heshima za mwisho.
Akitoa salamu za chama, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tabora, Saidi Nkumba, alieleza masikitiko makubwa kufuatia kifo cha kiongozi huyo, akisema chama na wananchi wamepata pigo kubwa.
Alibainisha kuwa,wanachama wa CCM na wakazi wa Mkoa wa Tabora kwa ujumla wameshtushwa na taarifa za kifo cha Kigalu, akimtaja kama kiongozi aliyekuwa mstari wa mbele kutetea maslahi ya wananchi wa Itilo na kusimamia maendeleo ya Halmashauri ya Mji Nzega kwa bidii na uadilifu.
“Hili ni pigo kwa Chama Cha Mapinduzi na Serikali. Tumempoteza mtu muhimu sana katika kipindi ambacho wananchi walikuwa wameanza kunufaika na utekelezaji wa ahadi alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29,mwaka jana,” alisema Nkumba.
Marehemu Kigalu anakumbukwa kwa mchango wake katika kuimarisha utoaji wa huduma za kijamii na kusukuma mbele ajenda za maendeleo katika kata yake na halmashauri kwa ujumla.
Kifo chake kimeacha pengo kubwa katika uongozi wa Kata ya Itilo na Halmashauri ya Mji Nzega, huku wananchi wakieleza masikitiko yao na kumwelezea kama kiongozi aliyekuwa karibu na jamii.
