DAR-Mwinjilisti na Mhubiri wa Kimataifa, Dkt. Alphonce Temba ameomba nafasi ya kuonana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kumshirikisha mikakati kabambe anayoamini itawezesha kuinua uchumi wa vijana, jamii na Taifa kwa ujumla.
Dkt. Temba amesema uzoefu alionao wa kuishi na kufanya kazi katika mataifa zaidi ya 10 barani Afrika, pamoja na kuwashauri baadhi ya viongozi wa Kiafrika, umemjengea uelewa mpana kuhusu masuala ya uongozi, biashara na maendeleo ya kiuchumi.
Amesema, uzoefu huo unamfanya aone umuhimu wa kushirikisha maono yake kwa Mheshimiwa Rais ili kuchangia jitihada za kuifanya Tanzania izidi kustawi na kusonga mbele kimaendeleo.
Dkt. Temba ameongeza kuwa, ana ujumbe maalum alioupokea kutoka kwa Mungu kwa ajili ya kumfikishia Rais Dkt.Samia, akisisitiza kuwa ujumbe huo una mwelekeo wa kuimarisha maendeleo ya Taifa.
Ameeleza imani yake kuwa,endapo ujumbe huo utapokelewa na kufanyiwa kazi, Mungu atanena na kunyoosha mkono wake, hali itakayochochea maendeleo endelevu nchini.
Aidha, amesema Tanzania ina fursa kubwa ya kufanya vizuri zaidi kiuchumi endapo itatumia kikamilifu rasilimali zake, maarifa, na nguvu kazi iliyopo, hususan vijana.
Kwa mujibu wa Dkt. Temba, Taifa lina uwezo wa kufikia viwango vya juu vya maendeleo kama ilivyo kwa mataifa makubwa duniani yakiwemo Marekani, Ujerumani, China na Australia, endapo mikakati sahihi ya kiuchumi na kijamii itawekwa na kutekelezwa ipasavyo.
Dkt. Temba amesisitiza kuwa,nia yake siyo binafsi, bali ni kuona Tanzania inanufaika na mawazo mapya, ushauri wa kitaalamu na misingi ya kiroho inayoweza kuchangia ustawi wa wananchi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Vilevile, Dkt.Temba amepongeza uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Uganda huku akisema ujio wa Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni ndani ndani ya muda mfupi baada ya ushindi wake ni ishara njema.
Amesema, hivi karibuni akiwa jijini Kampala nchini Uganda alishuhudia namna uchumi wa Taifa hilo unaendelea kukua kwa kasi kutokana na ujumuishaji wa wazawa na wageni katika shughuli za kiuchumi na uzalishaji.
Amesema,ukuaji wa uchumi wa Uganda unatokana kwa kiasi kikubwa na sera zake za wazi katika biashara, hususan namna ilivyofanikiwa kuwajumuisha wageni katika shughuli za kiuchumi.


Akizungumzia hotuba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu kuondolewa kwa vikwazo katika mipaka, Dkt. Temba amempongeza kwa kuyataja maono hayo kuwa ni ya kimkakati na yenye tija kubwa kwa uchumi wa Taifa.
Amesema, maamuzi hayo yataimarisha biashara za mipakani na kuongeza ushindani wa kiuchumi wa Tanzania katika ukanda wa Afrika Mashariki,Kusini na Kati.
Aidha, Dkt. Temba amesema,anamshukuru Mungu kwa kumuongoza Rais Samia na kwa kuyasikia maombi yake aliyokuwa akiomba kuhusu ukomo wa maandamano na mivutano nchini, hususan kuanzia Oktoba 29, 2025.
Amesema, Mungu alizuia mwendelezo wa maandamano na vurugu ili kumpa Rais Samia nafasi ya kuendelea kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo endelevu.
“Kitendo cha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuungana na Mheshimiwa Rais Museveni na kukiri kuwepo kwa vikwazo katika mipaka ni jambo kubwa sana. Hatua hii itawanufaisha Watanzania wengi, hasa wafanyabiashara wa mipakani,” amesema Dkt. Temba.
Akitolea mfano, amesema katika mpaka wa Tunduma kati ya Tanzania na Zambia, wapo Watanzania wengi wanaojihusisha na biashara, lakini hulazimika kutumia mipaka mingine kutokana na vikwazo na tabia za baadhi ya watu wanaowanyanyasa wafanyabiashara wa Kitanzania.
Dkt. Temba amesema, athari za vikwazo hivyo zimeifanya Tanzania kupoteza fursa za kiuchumi, akitolea mfano wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambako hapo awali wafanyabiashara wengi walikuwa wakija Tanzania kufanya biashara mbalimbali ikiwemo ya almasi na dhahabu.
Amesema, kutokana na vikwazo mipakani, wafanyabiashara hao waliamua kuelekeza shughuli zao nchini Uganda.
Ameongeza kuwa kwa sasa raia wa Congo, Rwanda, Ethiopia, Somalia na Eritrea wamejikita kwa wingi nchini Uganda wakifanya biashara, jambo lililochangia kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi wa Uganda na kukuza uchumi wa Taifa hilo.
Katika hatua nyingine, Dkt. Temba ameishauri Serikali ya Tanzania kubadili mtazamo katika kushughulikia wakimbizi, hususan raia wa Somalia wanaopita nchini kuelekea Afrika Kusini.
Amesema, kuwakamata, kuwafungulia kesi na kuwahukumu vifungo vya gerezani kunasababisha mzigo mkubwa wa gharama kwa Serikali.
Kwa mujibu wa Dkt. Temba, njia mbadala na yenye tija ni kuwatoza faini wale wanaobainika kuingia nchini kinyume cha sheria, kupita bila vibali au kuzidisha muda wa kukaa, kisha kuwapa saa 24 kuhakikisha wameondoka nchini kwa njia yoyote.
Amesisitiza kuwa, Serikali haipaswi kuingia gharama za kuwalisha au kuwasafirisha watu hao, hasa ikizingatiwa kuwa wengi wao hawana hati halali za kusafiria, hali ambayo husababisha matumizi makubwa yasiyo ya lazima na kudumaza uchumi.
Kwa ujumla, Dkt. Temba amesema endapo biashara zitafunguliwa kikamilifu katika mataifa jirani kama inavyoakisi maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, umaskini utapungua kwa kiwango kikubwa, vijana watapata fursa nyingi za kiuchumi, na Taifa litaingia katika hatua mpya ya maendeleo endelevu.
VIDEO ya Mwinjilisti Temba akiwa jijini Kampala nchini Uganda hivi karibuni.
