Profesa Shemdoe,menejimenti Lushoto wakutana kujipanga kutekeleza maelekezo ya Waziri Mkuu

TANGA-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amefanya kikao kazi na Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, kilicholenga kuweka mkakati wa utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba hususani ya utatuzi wa kero na changamoto za wananchi, aliyoyatoa Februari 17, 2026 wakati wa ziara yake wilayani Lushoto.
Katika kikao kazi hicho kilichofanyika Feberuari 18, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Prof. Shemdoe ameisisitiza Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kuhakikisha inasimamia kikamilifu utatuzi wa kero na changamoto zinazowakabili wananchi kama alivyoelekeza Mhe. Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba.

"Mmemsikia Mheshimiwa Waziri Mkuu akituasa tubadilike kiutendaji, tuachane na utendaji kazi wa mazoea, hivyo twendeni tukasikilize kero na changamoto zinazowakabili wananchi na tuzitatue kwa wakati," amesisitiza Prof. Shemdoe.
Prof. Shemdoe amefafanua kuwa, ufanyaji kazi wa mazoea wa kusikiliza kero za wananchi na kutozitatua ndio sababu kubwa ya watu wengi kujitokeza na kuwasilisha changamoto zao kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu katika mikutano yake na wengine wanakuwa wamesafiri umbali mrefu ili kuitafuta fursa hiyo, hivyo watumishi wanapaswa kubadilika na kutekeleza wajibu wao ipasavyo.

“Mkurugenzi tuone uwezekano wa kuwa na kliniki au mikutano ya kusikiliza kero za wananchi katika ngazi ya kata, naamini utaratibu huo utawezesha utatuzi wa kero nyingi za wananchi na utapunguza idadi ya wananchi watakaojitokeza kuwasilisha malalamiko yao kwenye mikutano ya viongozi wakuu wa kitaifa,” ameeleza Prof. Shemdoe.
Sanjari na hilo, Prof. Shemdoe ameipongeza Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kwa kumpa ushirikiano wa kiutendaji Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, na kuwataka kuendelea kumpa ushirikiano kwa ajili ya kuleta maendeleo katika halmashauri hiyo.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Dkt. Ikupa Mwasyoge ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya elimu na afya ambayo imeboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Prof. Shemdoe ameendelea kudhihirisha uchapakazi wake katika kutekeleza maelekezo ya viongozi wakuu wa kitaifa kwa kufanya kikao kazi hicho na Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, ikiwa ni siku moja tu baada ya Mhe. Waziri Mkuu kumsifu kwa utendaji kazi wake mbele ya wananchi wa Jimbo la Lushoto.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here