Rais Dkt.Mwinyi atoa wito kwa wafanyabiashara kuelekea Mwezi Mtukufu wa Ramadhani

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewataka wafanyabiashara kutopandisha bei za vyakula katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ili kuwaondolea ugumu waumini wanaojiandaa kufunga.
Wito huo ameutoa Februari 14,2026 huko Beltras, Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi kupitia hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mhe. Zubeir Ali Maulid katika Kongamano la Afrika Mashariki la kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Katika hotuba hiyo, Rais amesema, Ramadhani ni mwezi wa kipekee kwa Waislamu duniani kote, ambapo huungana kwa kufunga kwa lengo la kutimiza moja ya nguzo tano za Uislamu na kuthibitisha utiifu wao kwa Mwenyezi Mungu.
Amesisitiza kuwa, ni muhimu kwa wafanyabiashara kuonyesha huruma na mshikamano kwa waumini kwa kuepuka kupandisha bei za bidhaa muhimu

“Ramadhani inakaribia, hivyo wafanyabiashara wasipandishe bei za vyakula kwani kufanya hivyo kutawaongezea ugumu wanaofunga. Wapeni wepesi na upole wafungaji,” ilieleza sehemu ya hotuba hiyo.

Aidha, Rais amebainisha kuwa faida kubwa katika kipindi cha Ramadhani ni kuimarisha ibada, mshikamano na huruma miongoni mwa jamii, badala ya kuongeza faida za kibiashara kwa kuwaumiza wananchi.

Sambamba na hilo, amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani na utulivu nchini, akieleza kuwa amani ni nguzo muhimu ya maendeleo na ustawi wa wananchi, hususan katika kipindi hiki cha ibada.
Katika kongamano hilo, Spika alikipongeza Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar kwa juhudi zake za kusimamia misingi ya dini ya Kiislamu na kuendeleza kongamano hilo kila mwaka.

Pia aliwashukuru wadhamini na mashekhe kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki kwa kushiriki maandalizi ya Ramadhani, akiahidi kuwa Serikali itaendelea kuthamini mchango wao wa kidini.

Mapema, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera na Baraza la Wawakilishi), Mhe. Hamza Hassan Juma, alisema Serikali imeshatoa maelekezo kwa Kamisheni ya Utalii kuhakikisha wageni wanaokuja Zanzibar wanaheshimu Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Ameongeza kuwa, vyombo vya ulinzi na usalama vimeimarishwa ili kuhakikisha amani na utulivu vinadumu katika kipindi chote cha Ramadhani na nyakati nyingine.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here