Rais Dkt.Samia apongeza hatua zinazochukuliwa na Mahakama kuimarisha utoaji haki nchini

NA FAUSTINE KAPAMA
Mahakama Dodoma

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa hatua mbalimbali iliyochukua, ikiwemo utekelezaji wa miradi ya miundombinu, ugatuzi wa shughuli za Mahakama ya Rufani na kuimarisha utoaji haki nchini.
Meza Kuu inayoongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Emmanuel John Nchimbi ikiwa katika picha ya pamoja.

Mhe. Dkt. Samia ametoa pongezi hizo leo tarehe 02 Februari, 2026 kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Emmanuel John Nchimbi kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria 2026, yaliyofanyika kitaifa katika Viwanja vya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Akizungumzia utekelezaji wa miradi ya miundombinu, Rais Samia ameeleza kuwa majengo mengi yatakamilika mwezi Machi, 2026 na mengine mwezi Oktoba mwaka huu, hivyo akahimiza usimamizi wa miradi hiyo ili ikamilike kama ilivyopangwa na kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana.

Kadhalika, Mhe. Dkt. Samia ameonesha kufurahishwa na hatua zilizochukuliwa za ugatuzi wa shughuli za Mahakama ya Rufani kwa kuanzia na Kanda tano za Dar es Salaam, Mwanza, arusha, Mbeya na Tabora.

Aidha, Rais Samia ametambua jitihada za Mahakama za kuimarisha utoaji haki nchini kwa kutunga Kanuni mbalimbali zinazosaidia usikilizaji wa mashauri ya madai na jinai na katika kipindi kifupi cha miezi sita, Kanuni 11 imetungwa ili kuboresha upatikanaji wa haki hapa nchini.

"Napendekeza jitihada hizi ziende sambamba na usimamizi wa dhamana kwa wale watuhumiwa wenye stahiki za kisheria kupata haki mahakamani. Hili ni muhimu kwani linawezesha watuhumiwa kuendelea na shughuli za maendeleo wakiwa kwenye dhamana," ameeleza kwenye hotuba yake.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Emmanuel John Nchimbi [juu na chini] akizungumza kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria yaliyofanyika leo tarehe 02 Februari, 2026 Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Meza Kuu inayoongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Emmanuel John Nchimbi ikiwa katika picha ya pamoja. Picha chini ni sehemu nyingine ya Meza Kuu.

Rais Samia ametoa rai kwa Wadau wote wa Mahakama kuunga mkono jitihada hizo kwa ustawi wa Taifa kwa kuzingatia kuwa zoezi hilo la dhamana linahusisha pia Taasisi nyingine.

Kadhalika, Mhe. Dkt. Samia ameipongea Mahakama ya Tanzania kwa kuendelea kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano [TEHAMA] katika shughuli za utoaji haki na kiutawala pia.

‘Nimefurahi kusikia kuwa Mahakama imeanza ujenzi wa mfumo wa Akili Unde kwa ajili ya kuchukua mwenendo na kumbukumbu za mashauri mahakamani. Hii ni hatua nzuri na muhimu itakayosaidia kuleta ufanisi katika utoaji wa haki,’ amesema.

Amebainisha kuwa ili Mahakama iweze kuchangia kikamilifu katika ustawi na maendeleo ya Taifa, haina budi kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia.

Akizungumzia Kauli mbiu ya maadhimisho hayo inayosema, ‘Mchango wa Mahakama katika Ustawi na Maendeleo ya Taifa,’ Rais Samia ameeleza kuwa imebeba ujumbe muhimu unaonesha kuwa Mahakama si tu Mhimili uliojikita katika kutoa haki pekee, bali ni guzo muhimu ya ustawi wa jamii, maendeleo ya kiuchumi na ustawishaji wa amani ya Taifa.

‘Mahakama ndiyo Mhimili ambao unahakikisha kuwa haki inapatikana kwa wote bila upendeleo wala uonevu wa aina yoyote. Mahakama siyo tu chombo cha mwisho cha utoaji haki nchini, bali ni mshirika muhimu katika safari ya maendeleo ya Taifa,’ amesema.

Ametoa mfano kwa mwaka 2025 kuwa, Mahakama ilishughulikia mashauri ya kiuchumi yenye thamani ya zaidi ya Trioni 50 na kati ya hayo, mashauri yenye thamani ya trilioni 13 yalisikilizwa na kutolewa uamuzi kati ya mwezi Oktoba hadi Desemba, 2025 pekee.

Rais Samia amesema kuwa Mahakama inaposikiliza na kutoa uamuzi kwa wakati kwenye mashauri ya jinai inatoa mchango wake wa kuimarisha amani na utulivu wa jamii na hivyo kuwezesha kufanyika kwa shughuli za kiuchumi na kijamii.
Meza Kuu inayoongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Emmanuel John Nchimbi ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania (juu na chini).
Meza Kuu inayoongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Emmanuel John Nchimbi ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Picha chini ni Mawaziri waliohudhuria Maadhimisho hayo.
Meza Kuu inayoongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Emmanuel John Nchimbi ikiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Dini na Mila. Picha chini ni wawakilishi wa wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Meza Kuu inayoongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Emmanuel John Nchimbi ikiwa katika picha ya pamoja Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Mashtaka.
Meza Kuu inayoongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Emmanuel John Nchimbi ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania na Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria 2026 [juu na chini].
"Kwa kutambua umuhimu wa Mahakama katika ujenzi wa Taifa, Serikali imeendelea kuchukua hatua za makusudi katika kuimarisha uhuru wa Mahakama ili kuiwezesha kutekeleza wajibu wake kikamilifu na kuchochea ustawi na maendeleo yz Taifa. Lengo kuu la hatua hizi ikiwa ni sehemu ya kutekeleza dhamira ya Serikali ya kujenga Taifa lenye amani na uchumi jumuishi na imara," amesema.

Aidha, Mhe. Samia ameeleza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Mahakama katika ujenzi wa miundombinu ya Mahakama, kuimarisha rasimilimaliwatu na kuboresha maslahi ya watumishi wa Mahakama na kusogeza huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi, hususan kupitia mpango wa ujenzi wa Mahakama za Mwanzo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here