IRINGA-Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli, amewataka Wahandisi wa Umwagiliaji nchini kuachana na kufanya kazi kwa mazoea na badala yake kutumia mbinu bunifu na uzoefu wa kitaalamu katika kusimamia miradi ya umwagiliaji, ili kuhakikisha miradi hiyo inaleta tija kwa Taifa.
Akifungua mafunzo ya usimamizi wa mikataba, sheria za ununuzi na utafiti wa miamba katika mabwawa mkoani Iringa, Bw. Mweli amewataka wahandisi kufuta dhana ya kukariri kwa kuwa usimamizi wa wakandarasi unahitaji mbinu za ziada na kubadilishana uzoefu miongoni mwa wataalamu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na wadau wengine.“Utatuzi wa changamoto za miradi haujawahi kuandikwa wote kwenye makaratasi. Mara nyingine unakutana na mkandarasi mbishi, hapo ndipo unahitaji kuzungumza na mhandisi mwenzako aliyejua jinsi ya kumdhibiti. Msikae kama mnaogopana, kaeni pamoja mbadilishane mbinu za kiutendaji,” alisema Mweli.
Katibu Mkuu amebainisha kuwa mafunzo hayo, yanayofadhiliwa na Serikali kupitia Mradi wa TRIP 2 kwa ushirikiano na Benki ya Dunia, yanalenga kuwajengea uwezo wahandisi kufanya maamuzi sahihi katika hatua za usanifu na ujenzi ili kupunguza athari na kuboresha ubora wa miradi.Aidha, Mweli alisisitiza umuhimu wa watumishi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kuwa na uwezo mkubwa wa kuchambua taarifa za upembuzi yakinifu na kusimamia washauri waelekezi kwa umakini zaidi, ili miradi iwe na thamani ya fedha na kuleta matokeo makubwa.
Katika ziara yake mkoani Iringa, Mweli alitembelea Skimu ya Umwagiliaji Mkombozi yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 56 na kuipongeza Tume kwa kukamilisha mradi huo wa kimkakati, ambao tayari umeanza kunufaisha wakulima upande wa mashariki wa skimu hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Bw. Raymond Mndolwa, aliwataka wahandisi wa mikoa kusimamia kwa nidhamu miradi mikubwa 146 inayotekelezwa na Tume, akisisitiza umuhimu wa uelewa wa sheria za ununuzi, usimamizi wa mikataba na makusanyo ya mapato ya ndani.
“Tusipoboresha utendaji tutachekwa na ni hatari kwa Taifa. Simamieni uhandisi wenu kwa kujiamini na msikubali kupigwa na wakandarasi au washauri waelekezi. Msifanye kazi kwa kuogopa ukaguzi tu, ogopeni laana ya wananchi mnaowaachia miradi yenye mapungufu. Acheni miradi yenye matokeo mkumbukwe vizuri,” alisisitiza Mndolwa.
Aidha, Mndolwa amewataka watendaji kuzingatia suala la makusanyo ya mapato ya ndani, akieleza kuwa ni lazima kila mhandisi wa mkoa ahakikishe skimu zinalipa tozo.
“Mwaka huu hakuna ‘mswalia mtume’, lazima target za mapato zifikiwe ili Serikali iendelee kuwekeza. Kama watu wanatumia miundombinu ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na hawataki kulipa, funga maji,” aliongeza.
Viongozi hao pia wamehimiza wahandisi kushirikisha wananchi tangu hatua za awali za usanifu wa miradi ili kuepusha migogoro ya fidia, wakibainisha kuwa miradi ya Tume haina utaratibu wa kulipa fidia bali inahitaji ushirikishwaji wa jamii.
“Mafunzo haya yatachangia kuongeza ufanisi na ubora wa miradi ya umwagiliaji nchini, sambamba na kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji,” amesema Mndolwa.
Mafunzo hayo ya siku sita yanatarajiwa kuongeza ufanisi katika usimamizi wa miradi chini ya Mradi wa TRIP 2, ambao unahusisha ujenzi wa mabwawa ya kuzuia mafuriko yanayoathiri wanachi na eneo la Reli ya Kati na SGR ili kudhibiti mafuriko pamoja na miradi mingine ya kitaifa.
Tags
Habari
NIRC Tanzania
Sekta ya Kilimo Tanzania
Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC)
Watumishi NIRC










































