NA DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua rasmi Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa yaliyopo Kikombo mkoani Dodoma.
Taswira ya Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa (MMUT), Kikombo Mkoani Dodoma mara baada ya kuzinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 24 Februari, 2026.
Katika uzinduzi huo uliofanyika leo Februari 24,2026, Rais Dkt.Samia amesisitiza kuwa,ulinzi imara na amani endelevu ni msingi mkuu wa maendeleo ya taifa.
Amesema kuwa,hakuna uwekezaji unaoweza kustawi bila kuwepo kwa mazingira salama na tulivu.
Ameeleza kuwa, ustawi wa wananchi na ukuaji wa uchumi hutegemea kwa kiwango kikubwa hali ya amani na usalama wa nchi.
Matukio mbalimbali yakimuonesha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alipozindua rasmi Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa (MMUT), Kikombo Mkoani Dodoma tarehe 24 Februari, 2026.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Maafisa Askari, Watumishi wa umma na wageni mbalimbali waliohudhuria uzinduzi wa Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa (MMUT), Kikombo Mkoani Dodoma tarehe 24 Februari, 2026.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda, amesema, gharama zilizotumika kukamilisha ujenzi wa jengo hilo na miundombinu iliyopo ni Sh. 212 bilioni ambapo fedha zote zimetolewa na Serikali.
“Makao Makuu haya ya kudumu ya ulinzi wa taifa ni ya kwanza kabisa kihistoria katika jeshi letu. Kama wote mnavyojua, kabla ya makao makuu haya, jeshi lilikuwa na makao makuu yake Upanga, Dar es Salaam, tangu kuanzishwa kwake mwaka 1964,” amesema Jenerali Mkunda.
“Ni dhahiri kuwa hatuwezi kujenga taifa lenye ustawi wa kweli bila kuwa na misingi madhubuti ya ulinzi na amani. Uwekezaji, biashara na shughuli nyingine za kiuchumi hustawi pale ambapo kuna uhakika wa usalama,” amesema Rais Dkt.Samia.
Amebainisha kuwa, hivi karibuni shirika la kimataifa la tathmini ya ukuaji wa uchumi duniani, Moody's limeipatia Tanzania daraja la B1, kiwango alichokieleza kuwa ni chachu muhimu kwa mustakabali wa ukuaji wa uchumi na kuvutia uwekezaji zaidi.
Rais Samia amesisitiza kuwa,kadri taifa linavyoimarika kiuchumi, ndivyo inavyokuwa muhimu zaidi kuwekeza katika sekta ya ulinzi ili kulinda mafanikio yaliyopatikana. Amesema Serikali itaendelea kuliwezesha Jeshi kwa kuboresha mazingira ya kazi, ili liwe tayari wakati wote kutekeleza majukumu yake kwa weledi na ufanisi.
Aidha, ameeleza kuwa taifa linalotaka kuheshimiwa katika jumuiya ya kimataifa halina budi kuwa na taasisi imara za kulinda uhuru, mipaka, rasilimali na watu wake.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa majengo na vifaa ni nyenzo tu za kusaidia utendaji kazi, na kwamba nguvu ya Jeshi haipimwi kwa miundombinu pekee bali kwa maadili na uzalendo wa wanajeshi wake.
Katika hotuba yake, Rais alinukuu kauli ya Baba wa Taifa, Hayati Julius Kambarage Nyerere, aliyewahi kusema, “Moyo kabla ya silaha,” akifafanua kuwa msingi wa Jeshi imara ni moyo wa kizalendo, nidhamu, utii, weledi, dhamira safi, uadilifu na uaminifu kwa taifa.Ameongeza kuwa utii kwa mamlaka ya kikatiba na uaminifu kwa taifa ndiyo silaha ya kwanza ya Jeshi linaloheshimika. Amewataka viongozi, makamanda na askari kuendelea kuishi kwa misingi ya kiapo chao, huku wakijiepusha na mienendo inayoweza kuchafua heshima ya taasisi hiyo.
Rais Samia pia amesisitiza kuwa Watanzania wana imani kubwa na Jeshi lao, na kwamba imani hiyo ni dhamana wanayopewa kulinda kwa vitendo.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi wote kutekeleza wajibu wao wa kikatiba katika kulinda amani na utulivu wa nchi.
Akikumbusha juhudi za kuimarisha ulinzi na usalama, Rais amesema tarehe 15 Desemba, mwaka jana alipata fursa ya kufungua Mkutano wa Tisa wa Wakuu wa Majeshi ya Ulinzi na Makamanda uliofanyika mkoani Tanga, katika Kituo cha Square, uliobeba kaulimbiu isemayo, “Ulinzi imara na amani ndio msingi wa maendeleo ya nchi yetu.”Amesema kaulimbiu hiyo inadhihirisha ukweli kuwa kila hatua ya maendeleo iliyofikiwa na taifa imejengwa juu ya misingi ya utulivu, nidhamu na ulinzi thabiti wa wananchi.
Pia,amehitimisha kwa kusisitiza kuwa bila uimara wa hali ya ulinzi na usalama, isingewezekana kufikia mafanikio ya sasa katika nyanja mbalimbali za maendeleo.











