MKINGA-Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeendelea kuthitibisha kwa vitendo nia yake ya kujali na kuthamini wananchi kwa kuhakikisha inafikisha huduma nafuu ya umeme kwenye kila kijiji na kitongoji mkoani Tanga,ili huduma hiyo isaidie kubadilisha na kuboresha maisha ya wananchi mkoani humo.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka REA, ndugu Abdulrazack Mkomi wakati wa ziara ya uhamasishaji wananchi kujiunga na huduma ya umeme wilayani Mkinga mkoani Tanga.
Mkomi amewasisitiza wananchi kuwa waangalifu wakati wa kufanya malipo ya kujiunga na huduma ya umeme, akieleza kuwa gharama ya kuunganisha umeme vijijini ni shilingi 27,000 kwa makazi na shilingi 139,000 kwa mitambo na mashine au viwanda.
Pia,amesema malipo yote yanalipwa kwa kutumia namba ya kumbukumbu inayotumwa moja kwa moja kutoka TANESCO kwa njia ya meseji na si vinginevyo.
Aidha, uhamasishaji huo ulijikita zaidi katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kujiunga na huduma ya umeme na matumizi ya umeme yenye tija ikiwemo kuanzisha na kufanya biashara kama saluni, uchomeaji, viwanda na nyingine nyingi ambazo zitasaidia kuongeza ajira na kipato.
Halikadhalika wananchi wamehimizwa kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa miundominu ya umeme ikiwemo nguzo, nyaya na miundombinu mingine ya umeme ili kuepuka uharibifu unaoweza kusababisha kukatika kwa huduma ya umeme pamoja na kuhatarisha usalama wa watu na mali.































