Salamu za Jumapili:Sifa zake zi kinywani

NA LWAGA MWAMBANDE

NI wazi kuwa, kila mmoja wetu ana wajibu wa kuendeleza utamaduni wa kumsifu Mungu kwa kinywa na kwa matendo,tukitambua kuwa sifa ni silaha ya kiroho na ishara ya imani iliyo hai.
Kwani,neno la Mungu katika Biblia Takatifu kuanzia Agano la Kale hadi Agano Jipya, linasisitiza kuwa,sifa za Bwana hazipaswi kuondoka vinywani mwa watu wake, bila kujali hali au changamoto wanazokutana nazo.

Rejea katika maandiko matakatifu, Biblia inasema: “Sifa zake ziwe kinywani mwangu daima” (Zaburi 34:1), ikionesha wazi kuwa kumsifu Mungu si jambo la msimu bali ni mtindo wa maisha kwa kila mmoja wetu.

Kupitia sifa,tunamtambua Mungu kama mwenye enzi, rehema na uaminifu usioyumba, pia huleta faraja, matumaini na mabadiliko ya kiroho katika jamii.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, sifa zake zi kinywani ni mwaliko wa kudumisha shukrani, unyenyekevu na utiifu kwa Mungu, ili jamii ijengwe katika misingi ya imani, upendo na matumaini yanayotoka kwake. Endelea;

1. Nitamhimidi Bwana, nasema kila wakati,
Kwani anaweza Bwana, hilo nimethibitisha,
Wa kumshinda hakuna, ni mwanzo tena tamati,
Sifa zake zi kinywani, nitaziimba daima.

2. Uhai yeye anipa, naishi hata na chati,
Sinacho cha kuogopa, kinachonipiga nati,
Yote migumu mifupa, avunja hainipati,
Sifa zake zi kinywani, nitaziimba daima.

3. Ameshika leo yangu, yote yangu mikakati,
Anairuhusu Mungu, itimilike kwa hati,
Ona mafungu mafungu, mazuri kuzidi noti,
Sifa zake zi kinywani, nitaziimba daima.

4. Kuna muda napigika, hata mpenyo sipati,
Ni kama ninaanguka, laini kama tikiti,
Ninamtaja Rabuka, kimya hata kwa sauti,
Sifa zake zi kinywani, nitaziimba daima.

5. Sifa zako Mungu wangu, si za kuunda kamati,
Washika maisha yangu, kuzidi mwili na koti,
Ndiwe kila kitu kwangu, ninakwamini kwa dhati,
Sifa zake zi kinywani, nitaziimba daima.
(Zaburi 34:1)

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here