Salamu za Jumapili:Uliishi pendo lake

NA LWAGA MWAMBANDE

KILA mmoja wetu ana wajibu wa kuishi kwa kuongozwa na upendo wa Mungu, kwa kuzingatia maadili ya imani, kutenda mema, kusameheana na kudumisha amani.
Upendo wa Mungu unapotekelezwa katika maisha ya kila siku, hujenga umoja, haki na ustawi wa kweli miongoni mwa waumini na jamii kwa ujumla.

Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa,upendo wa Mungu una faida kubwa kwa mtu na jamii kwa ujumla, kwani hujenga amani ya moyo, huimarisha maadili, na kuimarisha mshikamano wa kijamii.

Rejea katika maandiko ya neno la Mungu, utaona maandiko matakatifu yanasisitiza kuwa,kuishi katika upendo wa Mungu ni msingi wa haki, msamaha na maendeleo ya kweli katika jamii. Endelea;

1. Wewe umebahatika, unavyoitwa na Mungu,
Majina ya kutukuka, akuinuavyo Mungu,
Anavyosema hakika, anamaanisha Mungu,
Unapendwa naye Mungu, uliishi pendo lake.

2. Waitwa kitakatifu, uishi kitakatifu,
Usifanye ya kukifu, kwako kusiwe uchafu,
Ila uwe ni nadhifu, Muumba ukimsifu,
Unapendwa naye Mungu, uliishi pendo lake.

3. Anakuita rafiki, nafasi yako kwa Mungu,
Jina hilo labariki, kuwa karibu na Mungu,
Urafiki wamiliki, kwake Mungu una fungu,
Unapendwa naye Mungu, uliishi pendo lake.

4. Mungu anavyokuita, wewe ni mteuliwa,
Kote kule unapita, naye umechaguliwa,
Heshima umeipata, hiyo ya kufurahiwa,
Unapendwa naye Mungu, uliishi pendo lake.

5. Wewe kwake wa pekee, umeumbwa kipekee,
Mbele na uendelee, na sifa umtolee,
Popote utokezee, simama umtetee,
Unapendwa naye Mungu, uliishi pendo lake.

6. Kateua mwili wako, makao hekalu lake,
Huo unao ujiko, ni mtakatifu kwake,
Kakuongeza upako, makao ya Roho wake,
Unapendwa naye Mungu, uliishi pendo lake.

7. Wewe ni mjumbe wake, kwa huduma duniani,
Amekupa kazi yake, kufanya madhabahuni,
Takatifu kazi yake, iwe yako maishani,
Unapendwa naye Mungu, uliishi pendo lake.

8. Mungu kakuweka huru, kote kule uendako,
Yaongoza yake nuru, na wala giza haliko,
Pendo pasipo ushuru, kutoka kwake ni lako,
Unapendwa naye Mungu, uliishi pendo lake.

9. Anakuita mwanaye, katika viumbe vyote,
Kwamba uko kama yeye, kwenye uumbaji wote,
Zidi andamana naye, yaache mengine yote,
Unapendwa naye Mungu, uliishi pendo lake.

10. Nafasi Mungu kakupa, kweli ameniinua,
Nawe heshima kumpa, vema sana ukajua,
Siyo kwamba wamlipa, wema wake watambua,
Unapendwa naye Mungu, uliishi pendo lake.

11. Akutie nguvu Mungu, na kukustahilisha,
Utumike wanguwangu, Muumba ukimkosha,
Uwe nalo lake wingu, huku ukimwadhimisha,
Unapendwa naye Mungu, uliishi pendo lake.

(Yohana 15:15, 1 Wathesalonike 1:4, Waefeso 2:10, 1 Wakorintho 6:19, Matendo ta Mitume 1:8, Wagalatia 3:26, Warumi 5:8, Yohana 8:36, 2 Wakorintho 5:17)

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here