Serikali kununua ndege mpya nane kuimarisha ATCL ndani na nje

NA GODFREY NNKO

SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan ina mpango wa kununua ndege nane mpya kati ya hizo nne aina ya Dash 8 Q400 zipo katika hatua mbalimbali za manunuzi ambapo mbili zipo katika hatua ya zabuni na mbili hatua ya kibali.
Hayo yamesemwa leo Februari 26,2026 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa wakati akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo vya habari mbalimbali nchini katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Msigwa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo alikuwa akizungumzia kuhusu utendaji wa Serikali katika siku 100 za uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.

"Serikali imeendelea kuwekeza katika ununuzi wa ndege mpya, kuboresha karakana za matengenezo, kuimarisha mazingira ya kazi na kutekeleza mikakati ya kuongeza ubora, usalama na ufanisi katika utoaji wa huduma za usafiri wa abiria na mizigo kwa njia ya anga.

"Katika kipindi cha mwaka 2024/25, Serikali ilikamilisha ununuzi wa ndege aina ya Boeing 787-8 Dreamliner iliyowasili tarehe 20 Agosti 2024, na kufanya ATCL kuwa na jumla ya ndege 16."

Aidha,Msigwa amesema mchakato wa manunuzi ya ndege hizo ukikamilika utafanya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kuwa na ndege zaidi ya 20.

Msigwa amefafanua kuwa, kati ya ndege 16 ambazo zinamilikiwa na Serikali zile za masafa marefu zipo nne zikiwemo Boeing 787-8 tatu na Boeing 767-300F ya mizigo moja.

Vilevile,masafa ya kati amesema zipo sita zikijumuisha Airbus A220-300 nne na Boeing 737 MAX 9 mbili huku masafa mafupi zikiwa sita ambazo ni Dash 8 Q400 tano na Dash 8 Q300.

"Kuongezeka kwa ndege hizi kumeiwezesha ATCL kupanua mtandao wa safari kwa kurejesha safari za Johannesburg, Mtwara na Iringa, pamoja na safari mpya kuelekea Pemba, Lagos, Kinshasa, Victoria Falls, Cape Town na Accra hivyo kuongeza safari kutoka vituo 23 mwaka 2020/21 hadi vituo 33 mwaka 2025/26."

Pia, amesema upanuzi huu umeimarisha uunganishwaji wa Tanzania na masoko ya kikanda na kimataifa, kuongeza uhakika wa usafiri wa anga, kukuza utalii wa ndani na nje ya nchi, pamoja na kuongeza fursa za biashara na mapato ya fedha za kigeni.

Hata hivyo, Msigwa amesema ndege hizo mpya nane kati ya hizo nne zinatarajiwa kuja mwaka huu na hizo zingine kabla ya mwaka 2030 zitakuwa tayari.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here