Serikali yajibu madai ya tuhuma za meli iliyokamatwa ikisafirisha dawa za kulevya ikipeperusha bendera ya Tanzania nchini El Salvador

NA GODFREY NNKO

SERIKALI imejibu tuhuma zinazohusiana na kukamatwa kwa meli ya FMS Eagle ambayo ilikuwa inapeperusha bendera ya Tanzania nchini El Salvador ikidaiwa kubeba tani 6.6 za dawa za kulevya aina ya cocaine.
Mabaharia wa meli ya FMS Eagle wakiwa nyuma ya mafurushi ya Cocaine chini ya ulinzi mkali nchini El Salvador. (Picha na Jeshi la Wanamaji la El Salvador).

Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa ametoa ufafanuzi huo leo Februari 26,2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo vya habari mbalimbali nchini katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Msigwa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo alikuwa akizungumzia kuhusu utendaji wa Serikali katika siku 100 za uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan

Ameeleza kuwa, Serikali ya Zanzibar ilishafuta usajili wa meli hiyo baada ya kukosa ushirikiano kutoka kwa wamiliki wake, hatua iliyofuatwa na kutozwa faini pamoja na kuwasiliana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Msigwa amesema, kwa mujibu wa kumbukumbu za usajili, meli hiyo ilisajiliwa Zanzibar. “Ni kweli kwamba meli hiyo ilisajiliwa Tanzania, lakini inamilikiwa na raia wa kigeni na ilikuwa ikifanya shughuli zake nje ya nchi. Kutokana na ukiukwaji wa kanuni na taratibu, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeanza kuchukua hatua stahiki na itatoa taarifa rasmi baadaye kuhusu hatua zaidi zitakazochukuliwa."

Pia, amefafanua kuwa, mara baada ya kupokelewa kwa taarifa za kukamatwa kwa meli hiyo Februari 17, 2026, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilichukua hatua za haraka na kuifuta katika daftari la usajili Februari 18, 2026.

Kutokana na hatua hiyo, meli hiyo kwa sasa haina tena usajili wa Zanzibar. Aidha, Serikali imeanza mchakato wa kuwafuatilia wamiliki wa meli hiyo ili kubaini chanzo na mazingira ya tukio hilo.

Aidha, katika hatua nyingine, kampuni inayohusika imepigwa faini ya dola za Marekani 20,000 kwa mujibu wa kanuni na taratibu za International Maritime Organization (IMO).

Vilevile, Msigwa ameongeza kuwa, hakuna Mtanzania hata mmoja aliyekuwemo ndani ya meli hiyo wakati wa tukio, akibainisha kuwa mabaharia wote waliokuwepo ni raia wa kigeni.

Mabaharia waliokamatwa wakiwa na shehena kubwa ya dawa za kulevya katika maji ya El Salvador ni 10 wakiwemo wanne kutoka nchini Colombia, watatu kutoka Nicaragua, wawili wa Panama na mmoja kutoka Ecuador.

Awali,Rais wa nchi hiyo ya Amerika ya Kati, Nayib Bukele, kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X alieleza kuwa, operesheni maalum ilifanikiwa kukamata meli ya tani 1,200 (DWT) ijulikanayo kama FMS Eagle iliyoundwa mwaka 1982 na iliyokuwa ikipeperusha bendera ya Tanzania.

Alisema kuwa, Jeshi la Wanamaji la El Salvador lilifanikiwa kuinasa meli hiyo zaidi ya kilomita 700 kutoka pwani ya nchi hiyo, ikiwa imebeba tani 6.6 za Cocaine zilizokuwa zimefichwa ndani ya matenki (ballast tanks).

Kwa mujibu wa Rais Bukele, operesheni hiyo ni ushindi mkubwa zaidi kuwahi kutokea dhidi ya biashara ya dawa za kulevya katika historia ya nchi hiyo.

Aliongeza kuwa,wapiga mbizi waliobobea walithibitisha kuwa mzigo huo ulikuwa umefichwa katika sehemu maalum zilizotengenezwa kwa siri ndani ya meli, jambo linaloashiria uwepo wa mtandao wa kimataifa uliopangwa kwa kiwango cha juu.

Mamlaka za usalama zilieleza kuwa, uchunguzi unaendelea ili kubaini wahusika wakuu wa mtandao huo pamoja na njia zilizotumika kusafirisha shehena hiyo.

Mabaharia wote waliokuwemo ndani ya meli hiyo wamewekwa chini ya ulinzi kwa ajili ya mahojiano na hatua zaidi za kisheria nchini El Salvador.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here